Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe.Queen Sendiga amesema Serikali imetoa jumla ya shilingi Bilioni 139 katika
sekta ya Umwagiliaji katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini mwaka wa fedha 2024/25.
Mhe. Sendiga ameyasema hayo wakati akifungua Maonesho ya 31 ya NaneNane Kanda ya Kaskazini, Agosti 05, 2025 katika Viwanja vya Themi Njiro, Arusha ambapo alikuwa mgeni rasmi.
"Sekta ya Umwagiliaji katika Mkoa wa Arusha unatekeleza miradi ya
miundombinu ya Umwagiliaji yenye thamani ya Bilioni 85.24, Mkoa wa Kilimanjaro
miradi yenye thamani ya bil.39.1 na Mkoa wa Manyara miradi yenye thamani ya
Shilingi bil.15.2," alisisitiza Mhe. Sendiga.
Aidha, Mhe. Sendiga amewataka wakulima
kubadilika kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuweza
kujipatia kipato kizuri wanapofanya shughuli
za kilimo.
Kwa upande mwingine amewaomba wadau na Taasisi mbalimbali wawafikie
wakulima, wavuvi na wafugaji ili watatue changamoto zao ili waongeze tija
katika sekta hizo.
Mbali na hayo, Mhe. Sendiga
amewakumbusha wananchi wote
kuchagua viongozi ambao watasimama bega kwa bega na wakulima .
Sanjari na hilo, amewaomba washiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa
amani, utulivu na bila kuruhusu mazingira ya kuwagawa watanzania kiitikadi,
kidini au kikabila.
Kauli mbiu ya maonesho ya NaneNane 2025, " Chagua viongozi Bora kwa
Maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi."
Na. Ruth Kyelula - Manyara RS
0 Maoni