Mwenyekiti wa Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele, amewataka wazalishaji wa
maudhui mtandaoni kuhakikisha kuwa taarifa za uchaguzi wanazoziweka kwenye kurasa zao za mitandao
ni za kweli na zisizokuwa na chembe ya upotoshaji.
Akizungumza leo Agosti 3,
2025 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa baina ya INEC na Wazalishaji wa
Maudhui Mtandaoni, Jaji Mwambegele ameeleza kwamba ukosefu wa umakini katika
utoaji wa habari wakati uchaguzi mkuu unaweza kuharibu na kuhatarisha amani na
utulivu wa nchi.
“Ni ukweli kwamba mitandao
hasa ya kijamii imekuwa ni chanzo muhimu cha habari kutokana na kuwa taarifa
zinazochakatwa kwenye mitandao zinapatikana kwa urahisi na kwa haraka hiyo basi
ni muhimu kuhakikisha habari hizo zinakuwa ni za kweli,” amesema Jaji
Mwambegele.
Jaji Mwambegela pia, amewaasa
Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni kuepuka
matumizi mabaya ya Akili Unde (AI) ambayo inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia
ovu kusambaza habari za upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii.
Kuhusiana na madai ya
kuwa idadi ya wapiga kura walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la kupiga
kura inawezekana kuwa si sahihi kutokana na uwezekano wa kuwapo watu waliokufa
kwenye daftari hilo Jaji Mwambegele amesema;
“Nikweli huenda kukawa na
watu waliokufa kwenye daftari la wapiga kura iwapo hatujapata taarifa za mpiga
kura aliyepoteza maisha lakini tukipata taarifa hiyo tutamuondoa, ila hata
hivyo hakuna mtu aliyekufa anaweza kupiga kura hivyo uwepo wao unajaza nafasi tu
hauathiri upigaji kura,” alisema Jaji Mwambegele.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani amesema tume imejiwekea utaratibu wa
kuvishirikisha vyombo vya habari katika mchakati mzima wa uendeshaji uchaguzi ili
kuweka uwazi na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu.
“Tunatarajia kupata
ushirikiano kutoka kwenu ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika kwa
amani na utulivu, na iwapo kutakuwa na changamoto, fuateni Sheria, Kanuni,
Miongozo, Taratibu na Maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na
INEC,” amesema Ramadhani.
0 Maoni