Watendaji wakuu wa
taasisi za umma wamepatiwa maagizo sita (6) yenye lengo la kuongeza ufanisi wa
taasisi wanazoziongoza na hivyo kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikali
kuu.
Maagizo hayo yaliyotolewa
jana Jumatatu, Julai 28, 2025, na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi. Dk. Moses
Kusiluka na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu, ni pamoja na kuimarisha
ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yasiyo na tija, pamoja na Kujenga
uwezo wa ndani wa taasisi kwa kuboresha rasilimali watu, teknolojia na
miundombinu.
Maagizo mengine ni
kuongeza faida kwa taasisi za kibiashara, kuboresha huduma kwa taasisi za
huduma, Kukumbatia matumizi ya TEHAMA, na kila taasisi kutekeleza Dira 2050 kwa
nafasi yake.
Maelekezo hayo yalitolewa
katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha, Mkoani Pwani wakati wa
ufunguzi wa mafunzo elekezi ya siku nne
kwa wakuu wa taasisi za umma yalioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina
kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.
Balozi Dk. Kusiluka
alisema katika mwaka huu mpya wa fedha angependa kuona taasisi za umma
zinaepuka matumizi yasiyo na tija, na kuelekeza fedha zaidi katika maeneo ya
vipaumbele vya kitaifa kama vile miundombinu, afya, elimu, na huduma za
kijamii.
“Watendaji Wakuu wanalo
jukumu la kuhakikisha taasisi zao zinaendeshwa kwa misingi ya ufanisi na
uwajibikaji mkubwa,” alisema Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa ufunguzi wa mafunzo
yaliyowaleta pamoja wakuu wa taasisi za umma 114.
Balozi Dk. Kusiluka
aliongeza kuwa ili taasisi za umma ziongeze ufanisi, zinapaswa kujenga uwezo wa ndani wa taasisi kwa
kuboresha rasilimali watu, teknolojia na miundombinu.
Aidha, alizitaka taasisi
za umma, kila moja kwa nafasi yake, kuhakikisha zinashiriki katika kufanikisha
Dira 2050.
Dira hii inalenga
kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu, yenye viwanda, mifumo
ya kiutawala yenye uwazi, na ustawi kwa wananchi wote.
“Tunatarajia pato la
Taifa kufikia $1 trilioni ifikapo 2050, huku pato la mtu mmoja mmoja likifia
$7,000, hii sio kazi ndogo lakini tuna kila sababu ya kufikia lengo,” alisema
Dk. Kusiluka.
Aliongeza: “Taasisi zetu
ni nguzo muhimu ya utekelezaji wa Dira hii, na mafanikio ya Taifa letu
yatategemea namna taasisi hizi zitakavyobadilika kifikra na kuendana na
mahitaji ya mabadiliko ya kimkakati,” alisisitiza.
Aidha alisema mafunzo
elekezi kwa wakuu wa taasisi za umma ni tukio muhimu ambalo linaakisi dhamira
ya Serikali ya kuimarisha utendaji kazi, uongozi bora na uwajibikaji katika
sekta ya umma.
Kwa upande wake Msajili
wa Hazina Bw. Mchechu, alisema anatarajia kuona taasisi za Umma zenye mwelekeo
wa kibiashara zinaongeza ufanisi wa kiutendaji, mapato na faida, na hivyo
kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali kuu.
“Taasisi hizi lazima
ziendeshe shughuli zao kwa misingi ya kibiashara, zenye ushindani, ubunifu na
tija ili kuchangia kikamilifu kwenye pato la taifa kupitia gawio na michango
mingine,” alisema Bw. Mchechu.
Hili, alisema, linakwenda
sanjari na kukumbatia matumizi ya TEHAMA na hivyo taasisi za umma zinapaswa
kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya uwekezaji katika TEHAMA na kuhakikisha
mifumo inasomana ili kuongeza ufanisi.
“Lazima tukumbatie
matumizi ya TEHAMA kikamilifu ili kuleta tija iliyotarajiwa,” alisema Bw.
Mchechu.
Aliongeza: “Mwisho wa
siku tunataka kuona taasisi za umma zenye mrengo wa biashara, zinajiendesha
kibiashara na hivyo kupunguza au kuondokana kabisa na utegemezi kutoka Serikali
kuu.”
Kwa upande wa taasisi za
huduma, Msajili wa Hazina alizitaka ziendelee
kuboresha huduma zao kwa wananchi – kwa ubora, kwa wakati na kwa gharama
nafuu.
“Huduma kwa umma si
fadhila bali ni haki yao, na taasisi zetu ni lazima ziwahudumie kwa weledi na
kujali mahitaji yao halisi,” alisema Bw. Mchechu.
0 Maoni