Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi (INEC) imetangaza rasmi kuwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, na Madiwani kwa Tanzania Bara utafanyika Jumatano,
tarehe 29 Oktoba, 2025.
Akizungumza leo katika
hafla ya uzinduzi wa ratiba ya uchaguzi iliyofanyika makao makuu ya Tume,
Njedengwa jijini Dodoma, Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs
Mwambegele amesema jumla ya wapiga kura waliojiandikisha ni 37,655,559, ikiwa
ni ongezeko la asilimia 26.55 kutoka wapiga kura 29,754,699 walioandikishwa
mwaka 2020.
Ratiba ya Uteuzi na Kampeni
Jaji Mwambegele ameeleza
kuwa utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais
utafanyika kuanzia 9 Agosti hadi 27 Agosti, 2025. Kwa wagombea ubunge na
udiwani, utoaji wa fomu utaanza 14 Agosti hadi 27 Agosti, 2025.
Tarehe 27 Agosti, 2025,
itakuwa ni siku rasmi ya uteuzi wa wagombea kwa nafasi zote; Rais na Makamu wa
Rais, Wabunge, na Madiwani.
Kampeni za uchaguzi kwa
Tanzania Bara zitaanza 28 Agosti hadi 28 Oktoba, 2025, huku kwa upande wa
Tanzania Zanzibar kampeni zitadumu hadi 27 Oktoba, 2025, ili kupisha zoezi la
kupiga kura ya mapema.
Katika jumla ya wapiga kura waliojiandikisha
Tanzania Bara inajumuisha
36,650,932, na upande wa Tanzania Zanzibar inajumuisha 1,004,627, ambapo
725,876 wameandikishwa na ZEC na 278,751 wameandikishwa na INEC kwa kuwa
hawakuwa na sifa za kuandikishwa na ZEC.
Kuhusu jinsia
Wanawake ni 18,943,455
(asilimia 50.31),
Wanaume ni 18,712,104
(asilimia 49.69),
Watu wenye ulemavu ni
49,174
Vituo vya Kupigia Kura
Jaji Mwambegele amesema
jumla ya vituo 99,911 vitatumika katika uchaguzi huu:
97,349 vitakuwa Tanzania
Bara, 2,562 vitakuwa Tanzania Zanzibar. Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia
22.49 kutoka vituo 81,567 vilivyotumika kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.
Wito kwa Wananchi,
Mwenyekiti wa INEC ametoa wito kwa wananchi na wadau wote wa uchaguzi kushiriki
kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi huku wakizingatia sheria, kanuni,
miongozo, na maelekezo yatakayotolewa na Tume.
"Ushiriki wa
wananchi ni kiini cha mafanikio ya uchaguzi huru na wa haki," amesisitiza
Jaji Mwambegele.
0 Maoni