Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kikiongozwa na Mwenyekiti wake Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kimeidhinisha kwa kishindo
marekebisho ya Katiba ya chama hicho ya mwaka 1977 (toleo la Mei 2025), baada
ya kura ya maoni kuonyesha uungwaji mkono wa asilimia 99.8 kutoka kwa wajumbe
wa Mkutano Maalum wa CCM uliofanyika kwa njia ya mtandao siku ya Jumamosi.
Kura hiyo ya kihistoria
imeonyesha mshikamano na umoja wa wanachama wa CCM, ambapo jumla ya wajumbe
1,915 kati ya 1,931 waliotarajiwa walishiriki katika upigaji kura hiyo ya ndani
ya chama.
Akitangaza matokeo ya
kura hiyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Idara ya Oganaizesheni, Issa
Haji Ussi Gavu, alisema:
“Idadi ya wajumbe
waliotakiwa kupiga kura ni 1,931. Waliopiga kura ni 1,915. Kura za ‘hapana’ ni
sifuri, zilizoharibika ni tatu, na kura za ‘ndiyo’ ni 1,912, sawa na asilimia
99.8 ya kura zote halali.”
Akizungumza kabla ya
upigaji kura, Mwenyekiti wa CCM Dkt. Samia aliwahakikishia wajumbe kuwa
marekebisho hayo ni madogo lakini ya kimkakati, yenye lengo la kuipa Kamati Kuu
uwezo wa kuongeza idadi ya wagombea wanaoingia katika hatua ya kura za maoni,
pasipo kuvuruga mfumo wa sasa wa uteuzi.
“Mabadiliko haya
hayalengi kubadili mfumo mzima, bali kuongeza unyumbufu unaoendana na mahitaji
ya sasa ya chama chetu,” alisema Dkt. Samia.
Marekebisho
yaliyopitishwa yanahusisha Ibara ya 105(7F) ya Katiba ya CCM, ambayo sasa
itairuhusu Kamati Kuu kuongeza idadi ya wagombea wa ubunge na ujumbe wa Baraza
la Wawakilishi katika hatua ya kura za maoni. Vilevile, Ibara ya 91(6C) kwa
upande wa nafasi za udiwani pia imefanyiwa marekebisho kwa mtiririko huo huo.
Rais Dkt. Samia pia
alitumia fursa hiyo kuwapongeza wajumbe kwa ushiriki wao mkubwa, akisema kuwa
hatua hiyo ni uthibitisho wa uimara wa misingi ya demokrasia ndani ya CCM.
“Ushiriki huu mkubwa
unaakisi imani yenu katika mchakato wa ndani wa chama chetu. Hii ni CCM mpya,
inayojibadilisha kwa wakati, lakini ikidumisha maadili na misingi yake,”
alisema.
Hata hivyo, alibainisha
kuwa mchakato wa kura za maoni kwa upande wa udiwani utaendelea kama kawaida,
kwani tayari umeshapita hatua ambayo imefanyiwa marekebisho.
Kwa hatua hiyo, CCM
inaonekana kujiandaa kwa nguvu mpya kuelekea uchaguzi mkuu ujao, huku
ikihakikisha kuwa michakato yake ya ndani inaendana na mabadiliko ya kisiasa na
kijamii nchini.
0 Maoni