Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2050 Julai 17, 2025 jijini Dodoma, kufuatia kukamilika kwa
mchakato wa dira hiyo ya 2050 ya Tanzania Tuitakayo.
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo ameyasema hayo leo jijini
Dar es Salaam alipokutana na Jukwaa la Wahariri Tanzania kuelezea kuhusu
maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yalipofikia.
“Dira ya Taifa ya
2050 imepitia hatua 13, sasa imeshakamilika rasmi ambapo Mhe. Rais Samia Suluhu
Hassan ataizindua rasmi Julai 17, 2025 jijini Dodoma katika ukumbi wa Jakaya
Kikwete Convention Centre,” alisema Prof. Mkumbo.
Ameeleza kwamba,
katika kuhakikisha kuwa dira hiyo inatekelezwa na awamu zote zitakazokuja hadi
kufikia 2050, Rais Samia alimuagiza kuiwasilisha bungeni dira hiyo kwa ajili ya
kuidhinishwa na bunge, na alifanya hivyo katika kikao cha mwisho cha bunge
lililomaliza muda wake.
“Tumepeleka Dira ya
2050 bungeni ili kuhakikishakuwa hakuna kiongozi atakayeingia madarakani na
kuamua kuacha kuitekeleza Dira ya 2050 na kuja na mipango yake mingine…labda
arudi tena bungeni kuomba ridhaa ya kufanya mabadiliko,” alisema Prof. Mkumbo.
Ameongeza kuwa pia, wao
kama wanasiasa wamekubaliana kuhakikisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
inatekelezwa kwa kuhakikisha kila chama kinakuwa na Ilani ambayo inaakisi mambo
yaliyomo kwenye dira hiyo.
Amesema kuwa dira
hiyo imeshirikisha watu wa makundi mbalimbali wapatao milioni 1.2 ambapo katika
yao kundi kubwa lilikuwa la vijana, pia waliwafikia viongozi wastaafu na walio
madarakani 44 ili kupata mchango wao.
Pamoja na mambo
mengine, Prof. Mkumbo amesema kwamba Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itaanza
kutumika Julai mosi 2026, baada ya kumalizika kwa Dira ya sasa June 31, 2026,
hivyo serikali inamuda wa kutosha wa kujiandaa kwa utekelezaji wake.
0 Maoni