Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro Abdul-razaq Badru amewataka askari wa uhifadhi wa taasisi hiyo
kuendelea kulinda rasilimali za wanyamapori, Misitu na malikale kwa ari na
weledi ili taifa liendelee kunufaika na rasilimali hizo.
Kamishna Badru ametoa
maelekezo hiyo katika kilele cha siku ya
askari wanyamapori duniani (World
Rangers Day) leo tarehe 31 Julai, 2025 ambapo mamlaka hiyo imedhimisha siku
hiyo katika viwanja vya mnadani Karatu Mkoani Arusha.
Amesema mamlaka inatambua
mchango wa askari wa uhifadhi kutokana na kujitoa kwao kulinda rasilimali hizo
hivyo iko tayari kuboresha utendaji wao ili uendane na mabadiliko ya sayansi na
teknolojia. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kutambua mchango huo imewapa
vyeti na fedha kufuatia juhudi na kujitoa kwao katika ulinzi wa kupambana na
vitendo vya ujangili hali iliyosaidia kuokoa rasilimali za wanyamapori, mali za
shirika na askari wengine.
“Maadhimisho haya ni
maalum kwa ajili ya kutambua na kuenzi mchango wa askari wanyamapori wanaolinda
hifadhi na rasilimali zilizopo, Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa yenye
urithi mkubwa wa bioanuai, inao wajibu wa kuwaenzi askari wa uhifadhi ambao ni
mashujaa wetu wa ulinzi wa wanyamapori na misitu kwa maslahi ya nchi yetu na
vizazi vijavyo,” alisema Kamishna Badru.
Akielezea maadhimisho ya
siku hiyo Kaimu Meneja Idara ya Huduma za Ulinzi Mhifadhi Mwandamizi Linus
Tiotem ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro jumla
ya askari 11 wamepoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujangili,
ujambazi na kuuawa na wanyamaopri.
Siku ya Askari wa
Wanyamapori Duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 2007 kwa lengo la kuwakumbuka
askari waliopoteza maisha wakati wa kutekeleza majukumu yao, kauli mbiu ya
maashimisho ya mwaka huu ni “ Rangers: Powering Transformative
Conservation” ikilenga kuutambua mchango
wa askari wa Wanyamapori katika kuleta mabadiliko ya kweli katika uhifadhi wa
maliasili ambayo ni urithi wa Taifa.
Na. Kassim Nyaki - NCAA
0 Maoni