Wakala wa Vipimo (WMA) unaendesha zoezi la kuhakiki mita za umeme zilizofungwa katika viwanda mbalimbali nchini ili kuhakikisha Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inapata mapato stahiki na wenye viwanda wanalipa gharama stahiki kulingana na huduma ya umeme wanaotumia.
Hayo yalibainishwa jana Juni 18, 2025 na Meneja wa WMA Makao Makuu, Albogast Kajungu wakati akizungumza
na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
yanayoendelea katika uwanja wa Chinangali, Dodoma.
Kajungu alisema kuwa
hadi sasa WMA imekagua mita za umeme zaidi ya 2,000 huku lengo likiwa ni
kuhakiki mita zote zilizo kwenye matumizi katika viwanda vyote nchini katika
zoezi lililoanza Mei mwaka huu.
“Hali inaonesha
kwamba mita nyingi zilizo kwenye matumizi viwandani ziko vizuri. Chache ambazo
tumekuta zina mapungufu, tumewasiliana na Mamlaka husika kwa ajili ya
kuzirekebisha na nyingine kuzibadilisha ili kuhakikisha vipimo viko sahihi
kwenye eneo hilo,” alisema Kajungu.
Akieleza zaidi,
alisema kuwa zoezi hilo la uhakiki linahusisha mita zote za umeme zilizo katika
matumizi lakini Wakala imeona ianze na zile zilizoko viwandani kwakuwa
zinatumia umeme mkubwa hivyo ikiwa haziko sawasawa, kuna uwezekano wa TANESCO
au wenye viwanda kupata hasara.
Aidha, alieleza kuwa
zoezi la uhakiki linahusisha pia bidhaa za chuma hususan zinazotumika katika
ujenzi kwani kumekuwa na malalamiko katika eneo hilo.
Akifafanua, Kajungu
alisema kuwa sekta ya ujenzi hapa nchini inakua kwa kasi ambapo miradi mingi ya
ujenzi inayotekelezwa na serikali inatumia bidhaa za chuma hivyo WMA imeona
iongeze nguvu kuhakiki bidhaa hizo hususani zinazozalishwa kwenye viwanda vya
ndani ili kuhakikisha zina vipimo vilivyo sahihi.
Alisema kuwa
wazalishaji wanajitahidi kuzalisha kwa kuzingatia viwango lakini lengo la
Wakala hiyo ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi zinaendelea kuwa
na vipimo sahihi ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ambayo yanaweza
kutokea kwa kutumia bidhaa za chuma ambazo hazikidhi vipimo vinavyokubalika
kisheria.
Sambamba na uhakiki
wa mita za umeme na bidhaa za chuma, Kajungu alieleza kuwa zoezi hilo la
uhakiki pia linahusisha dira za maji zilizo kwenye matumizi kwakuwa ndizo zenye
malalamiko yanayohusiana na bili na mengineyo.
Hata hivyo,
alibainisha kuwa pamoja na kuhakiki bidhaa zilizo kwenye matumizi, WMA kupitia
Kituo cha Vipimo Misugusugu kilichopo mkoani Pwani, pamoja na kazi nyingine,
huhakiki mita mpya za umeme na dira mpya za maji ili zinapokwenda kufungwa kwa
wateja ziwe zimeshathibitishwa kuwa vipimo vyake ni sahihi.
Kajungu alitumia
fursa hiyo kuwaalika wananchi wafike kwa wingi kwenye Banda la Wakala wa Vipimo
ili kujipatia elimu kuhusiana na vipimo mbalimbali vinavyotumika ili kuwalinda
kwa maana ya kupata thamani ya fedha wanazotoa wanapokwenda kununua bidhaa.
Wakala wa Vipimo ni
mojawapo ya Wakala za Serikali yenye dhima ya kutoa huduma za kumlinda mlaji
kupitia uhakiki wa vipimo, usimamizi wa vipimo na kutoa ushauri wa kitaalamu
kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Majukumu yake ni
kumlinda mlaji na umma kwa ujumla kupitia uhakiki na uthibiti wa vipimo
vinavyotumika katika biashara na huduma nyingine ili kuhakikisha kuwa vipimo
hivyo ni sahihi na vinatumika kwa usahihi kulingana na Sheria ya Vipimo Sura
340, mapitio ya mwaka 2002 na maboresho yake ya mwaka 2026
pamoja na kanuni zake.
0 Maoni