Mmiliki wa mbwa Preye
Maxwell anaonekana mwenye huzuni anapomuacha mbwa wake mpendwa Hanks katika
hifadhi ya wanyama katika jijini Lagos ambalo ni kitovu cha biashara cha
Nigeria.
Akibubujikwa na machozi,
anasema: "Siwezi kumudu kumtunza. Siwezi kumlisha kwa njia anayostahili
kulishwa."
Mbwa huyo wa miaka
miwili aina ya American Eskimo anabweka wakati mmiliki wake anageuka na
kuondoka katika Taasisi ya Uokoaji Wanyama ya St Mark’s iliyoko katika
kitongoji cha Ajah, Lagos.
Dkt. Mark Afua,
daktari wa wanyama na mwenyekiti wa kituo hicho cha uokoaji, anamchukua Hanks
na kumuweka kwenye kizimba cha banda kubwa la chuma, katika moja ya vyumba
vingi vya jengo la ghorofa moja lililoundwa kwa ajili ya kuhifadhiwa mbwa,
paka, nyoka na wanyama wengine.
Maxwell, mtaalamu wa
mikakati ya vyombo vya habari mtandaoni, alipoteza ajira hivi karibuni.
Kutafuta kazi kumemfanya asiwepo nyumbani mara nyingi, na hivyo kuhisi hawezi
kumtunza Hanks ipasavyo.
Uamuzi wa kijana huyo
mwenye umri wa miaka 33 haukuwa rahisi, lakini ni hatua ambayo wamiliki wengi
wa wanyama wa nyumbani wanachukua kutokana na kupanda kwa gharama za maisha
nchini Nigeria.
Taifa hilo lenye watu
wengi zaidi barani Afrika limekumbwa na mfumuko mkubwa wa bei tangu Rais Bola
Tinubu aingie madarakani miaka miwili iliyopita na kuondoa ruzuku ya mafuta
ambayo ilikuwa ikitumika kwa muda mrefu.
0 Maoni