Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kimemtunuku Shahada ya heshima Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) anayemaliza muda wake, Dkt. Akinwumi Adesina.
Dkt. Adesina
ametunukiwa Shahada ya Falsafa ya Sayansi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na Rais wa awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
katika mahafali ya 55, duru ya kwanza ya Chuo hicho, yaliyofanyika kwenye Ukumbi
wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Akisoma wasifu wa
Dkt. Adesina kabla ya kutunukiwa Shahada hiyo Prof. Rwekaza Mukandala ameleza
kuwa Dkt. Adesina ni mfano halisi wa muunganiko nadra wa taaluma bora, uongozi
wenye maono na athari chanya katika maisha, sifa ambazo zinamfanya kutunukiwa
shahada hiyo ya heshima.
Chuo hicho
kimejiwekea utaratibu wa kutunuku shahada za heshima kwa watu wenye sifa na
kukidhi vigezo kila baada ya miaka mitatu, kilimtunuku shahada hiyo Dkt.
Adesina baada ya kutoa mchango mkubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla
katika eneo la Kilimo na fedha.
Prof. Mukandala
alisema Dkt. Adesina mwenye shahada ya uzamivu ya Uchumi wa Kilimo ametoa
mchango mkubwa katika mageuzi kwenye sekta za kilimo, Uchumi na fedha barani
Afrika na kutolea mfano kuwa alipokuwa Waziri wa Kilimo nchini Nigeria mwaka 2011
alibuni mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango wa kuwapelekea
wakulima ruzuku ya mbolea kwa njia ya kieletronoki kupitia simu za mkononi
(e-wallet).
Alisema Mpango huo
uliongeza tija katika sekta ya kilimo na kunufaisha zaidi ya wakulima milioni
11 kwa kuondoa ukiritimba na rushwa kwa watu wa kati wasio waadilifu.
Kuhusu mageuzi ya
kiuchumi, Rais wa Benki ya AfDB baada ya kushika nafasi hiyo mwaka 2015
aliiwezesha benki hiyo kuongeza mtaji kutoka Dola za Marekani bilioni 93 mwaka
2015 hadi bilioni 208 mwaka 2019 ambapo chini ya uongozi wake alianzisha
vipaumbele vitano vikijulikana kama 5’s yaani, Angaza na ipe nishati Afrika,
lishe Afrika, kuza viwanda Afrika, Jumuisha Afrika na boresha maisha ya
waafrika na kwamba vipaumbele hivyo vinasifika
kwa kuleta athari chanya kwa watu zaidi ya milioni 565 barani Afrika.
Prof. Mukandala
aliongeza kuwa wakati wa uongozi wake AfDB imekuwa benki kinara ya kufadhili
miradi ya miuondombinu ambapo zaidi ya Dola za Marekani bilioni 55 zimetumika
katika sekta ya miundombinu barani Afrika.
Alisema kuwa Benki
hiyo katika uongozi wake, iliwekeza katika miradi ya usalama wa chakula ambapo
inaelezwa kuwa zaidi ya watu milioni 100 walinufaika na mradi huo. Zaidi ya
hapo, Benki hiyo ilitoa Dola za Marekani bilioni 3 kwa ajili ya kuimarisha
sekta ya afya barani Afrika na nyingine kama hizo kwa ajili ya kuimarisha sekta
ya dawa.
Kuhusu mageuzi ya
kifedha, Dkt. Adesina licha ya kuwa mchumi wa kilimo, lakini ametoa mchango
mkubwa kubadaili mifumo ya kifedha barani Afrika ili iwe jumuishi na
kuwanufaisha makundi ya watu wa aina zote wakiwemo vijana, wanawake na
wanavijiji.
Akiwa Rais wa AfDB
alisanifu upya mifumo ya fedha ya ugharamiaji
maendeleo barani Afrika kama kuongeza mtaji wa benki hiyo, kuzindua hati
fungani ya jamii na kuanzisha mifuko ya dharura ya kukabiliana na majanga.
Hatua zinazotajwa kuimarisha miradi ya miundombinu, afya, kilimo na nishati
barani Afrika.
Kwa upande wa
Tanzania, chini ya uongozi wake, AfDB imekuwa na ushirikiano mzuri na Serikalis
katika mkakati wa kuimarisha miundombinu ili kujenga uchumi shindani na
kuboresha sekta binafsi kwa ajili ya kuzalisha ajira. Kwa upande wa
miundombinu, AfDB inasaidia uendelezaji wa miradi ya usafiri wa ardhini, majini
na angani kama vile mradi Barabara ya mzunguko jijini Dodoma, ujenzi wa Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, kipande
cha kuunganisha Tanzania na Burundi.
Kuhusu kuimarisha
sekta binafsi, AfDB imekuwa mdau muhimu wa Tanzania katika kuimarisha sekta ya
kilimo ambayo imeiwezesha Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128.
AfDB pia inashirikiana na Tanzania katika kuendeleza Mradi wa Jenga Kesho iliyo
bora (BBT) ambao umewawezesha vijana zaidi ya 11,000 kujishughulisha na kilimo
cha kisasa nchini.
Akizungumza baada ya
kupokea Shahada hiyo ya heshima, Dkt. Adesina ambaye ametajwa yeye na benki
yake kama wadau wakubwa wa Tanzania, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumwalika kuja Tanzania, nchi
ambayo amesema anaipenda na kwamba yeye ni mwananchi wa Tanzania.
Aidha, amekishukuru
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa heshima waliyompatia na kuwasisitiza wanafunzi
takribani 842 waliotunukiwa shahada pamoja naye, kutumia maarifa waliyoyapata,
kubuni mikakati ya kulipeleka mbele Bara la Afrika.
0 Maoni