WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawathamini Watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye ualbino na wakati wote itahakikisha inawalinda na kuwapatia fursa stahiki katika ujenzi wa Taifa.
Amesema katika kuendelea kutekeleza mpango wa uwezeshaji wananchi
kiuchumi kwa kutumia mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, hadi
kufikia Machi, 2025 tayari shilingi bilioni 5.48 zimetolewa kwa vikundi 891 vya
Watu Wenye Ulemavu nchini.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mahsusi za
kuimarisha ustawi na utoaji huduma kwa watu wenye ualbino ikiwemo kuwatambua,
kuimarisha mifumo ya kisera na kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu hapa
nchini.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa (Juni 13, 2025) wakati
alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya
Kimataifa ya Uelewa kuhusu Ualbino yaliyofanyika katika uwanja wa Mwanga
Centre, mkoani Kigoma.
Ameongeza kuwa katika mwaka 2024/2025 kiasi cha ruzuku inayotolewa
kwa Vyama vya Watu wenye Ulemavu kimeongezeka hadi kufikia shilingi milioni 230
ikilinganishwa na shilingi milioni 200 zilizotolewa kwa mwaka 2023/2024.
Akizungumza kuhusu kuimarika kwa utoaji wa huduma za afya kwa watu
wenye Ualbino, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kwa kipindi cha kuanzia Julai
2021 hadi Juni 2024 Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ilitumia zaidi ya
shilingi milioni 500 kusambaza katika mikoa yote 26 ya Tanzania mafuta kinga ya
saratani ya ngozi kwa Watu wenye Ualbino.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ilitenga shilingi bilioni
8.743 kwa ajili ya huduma za ustawi wa Jamii na shilingi 182. 8 kwa ajili ya
ununuzi wa mafuta kinga ya saratani ya ngozi kwa watu wenye Ualbino”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa
wahakikishe wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki
na Ustawi kwa Watu wenye Ualbino, Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi na
Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Taarifa za Watu wenye Ulemavu (PD-MIS)
katika ngazi ya Halmashauri.
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa kupitia
maadhimisho hayo, Serikali imezindua programu janja ‘Albino Mobile App’ ambayo
itawezesha kufanya usajili na ukusanyaji wa taarifa za watu wenye ualbino kwa
njia ya kidigitali.
Amesema kuwa mfumo huo utarahisisha, utaharakisha na utahakikisha
usahihi katika usajili wa watu wenye ualbino na ulemavu nchini Tanzania,
hususan walioko maeneo ya pembezoni. “Mfumo huu utapunguza gharama za usafiri
na usafirishaji wa vifaa kwa ajili ya usajili, na pia kuwezesha upatikanaji wa
takwimu sahihi zinazosaidia Serikali kupanga na kutekeleza sera kwa ufanisi.”
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS)
Godson Mollel Amesema kuwa Serikali imefanya mambo makubwa yenye lengo la
kuwawezesha watu wenye Albino nchini ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kununua
mafuta kinga ambayo hugawiwa bure.
“Pia, Serikali imetoa agizo kwa halmashauri kutoa fedha kwa ajili
ya kununua mafuta kinga ambayo imesaidia kupunguza uhaba wa mafuta kinga.”
Pia, Godson amewataka watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi
kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika
Oktoba 2025 “Jitokezeni kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu, mkifanya
hivyo mtakuwa mmetimiza haki yenu ya kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa.”
Katika Maadhisho hayo Mheshimiwa Majaliwa alizundua Programu janja
ya usajili ya wenye ualbino ‘Albino Mobile App’. itakayowezesha kuwasajili na
kuwatambua wenye ualbino.
0 Maoni