Tume ya Madini
imeendelea kunadi fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya madini kupitia
ushiriki wake kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea
kufanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa
kutoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la Tume ya Madini, Afisa kutoka
Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Bw. Ashen Mwambage, amesema kuwa
sekta ya madini nchini imejaa fursa lukuki zikiwemo utafutaji na uchimbaji wa
madini, uanzishaji wa viwanda vya uongezaji thamani madini, biashara ya madini,
pamoja na usambazaji wa vifaa na huduma kwenye migodi.
“Tume ya Madini
inawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kushirikiana nasi katika kuendeleza
sekta hii kwa kushiriki katika maeneo mbalimbali ikiwemo ubia katika baadhi ya
leseni za madini,” ameema Mwambage.
Aidha, ametumia fursa
ya maonesho hayo kuhamasisha jamii kujitokeza kupata elimu kuhusu sekta ya
madini pamoja na kuelewa jinsi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli
zinazochochea maendeleo ya uchumi wa taifa kupitia rasilimali madini.
Tume ya Madini imekuwa
mstari wa mbele katika kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa sekta ya madini
nchini huku ikijizatiti kuvutia wawekezaji zaidi ili kuchochea ukuaji wa pato
la taifa na kuinua maisha ya wananchi.
0 Maoni