Mlima wa volkano wa
Lewotobi Laki Laki uliopo katikati mwa Indonesia ulilipuka Jumanne jioni na
kutema wingu kubwa la majivu moto hadi umbali wa kilomita 11 juu ya anga, hali
iliyosababisha usumbufu mkubwa wa safari za ndege kuelekea na kutoka kisiwa
maarufu cha utalii cha Bali.
Kwa mujibu wa taarifa
ya Wakala wa Jiolojia wa nchi hiyo, mlipuko huo ulitokea saa 11:35 jioni kwa
saa za huko, ambapo moshi wenye umbo la uyoga wa rangi ya machungwa ulifunika
kijiji cha Talibura kilichopo karibu na mlima huo, huku mashuhuda wakiripoti
kuuona moshi huo hadi umbali wa kilomita 150.
Mamlaka za Indonesia
zimetangaza hali ya tahadhari ya juu kabisa na kuwaonya watalii na wakazi kukaa
mbali na eneo hilo kwa sababu za kiusalama.
Kutokana na tukio
hilo, safari kadhaa za ndege zimesitishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Denpasar, Bali. Tovuti ya uwanja huo imeeleza kuwa sababu ya usumbufu huo ni
"kutokana na mlipuko wa volkano".
Safari zilizohusika
ni pamoja na zile za ndani kuelekea Jakarta na Lombok, pamoja na za kimataifa
kwenda nchi za Australia, China, India, Malaysia, New Zealand na Singapore.
Mamlaka zinaendelea
kufuatilia hali hiyo kwa karibu huku juhudi za kuwaokoa watu walioko katika
maeneo hatarishi zikiendelea.
0 Maoni