Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA) limefanikiwa kunyakua jumla ya tuzo 7 katika mashindano
ya kimataifa ya World Travel Awards, mafanikio makubwa na ya kihistoria ambayo
yanaonyesha dhamira thabiti ya TANAPA katika kulinda, kuhifadhi na kukuza
utalii wa ndani na wa kimataifa.
TANAPA kupitia
hifadhi zake 7 zimeshida tuzo hizo ambapo Hifadhi ya Taifa Serengeti imeibuka
mshindi katika tuzo za World Travel Awards katika kipengele cha Hifadhi Bora
Barani Afrika (Africa’s Leading National Park), ikiwa ni mara ya saba mfululizo
kushinda tuzo hiyo ya kifahari. Ushindi huu unaonesha ubora na mvuto wa hifadhi
hiyo maarufu duniani kwa uoto wake wa asili na uhamaji wa wanyamapori (The
Great Migration), jambo linaloendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya utalii
wa kimataifa.
Pia, Hifadhi ya Taifa
Mlima Kilimanjaro imetwaa tuzo la Hifadhi Bora ya Milima Barani Afrika
(Africa’s Leading Mountain National Park), kutokana na kuwapo kwa mlima mrefu
zaidi barani Afrika – Mlima Kilimanjaro ambao huvutia maelfu ya watalii na
wapanda milima kutoka kona mbalimbali za dunia.
Hifadhi ya Taifa Nyerere
nayo haikubaki nyuma, ambapo imeshinda tuzo ya Hifadhi Bora kwa Mandhari ya
Kuvutia Barani Afrika (Africa’s Leading Scenic National Park ), ikionyesha
jinsi TANAPA inavyoendelea kuhifadhi na kutangaza maeneo yenye thamani ya
kitalii na kihistoria.
Katika mwendelezo
huo, Hifadhi ya Taifa Tarangire imeibuka
mshindi katika kipengele cha Hifadhi Bora kwa Utalii wa Tembo, Hifadhi
ya Taifa Serengeti kwa mara nyingine kuwa Hifadhi inayoongoza kwa kivutio cha
wanyama wakubwa watano (Big Five) , Hifadhi ya Taifa Ruaha kuwa Hifadhi
inayoongoza kwa utalii wa kitamaduni Barani Afrika na Hifadhi ya Taifa Kitulo
Hifadhi bora kwa fungate Barani Afrika.
Ushindi wa hifadhi
hizi siyo tu kwamba ni fahari kwa Taifa, bali ni nyenzo muhimu katika
kujitangaza kimataifa, kuvutia watalii, na kuongeza mapato ya fedha za kigeni
kupitia sekta ya utalii. Tuzo hizi zinaimarisha nafasi ya Tanzania kama
kiongozi wa utalii duniani, pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu
ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufahamika kwa
vivutio hivyo utatangaza fursa za uwekezaji nchini, hususan katika
maeneo ya Hifadhi za Taifa 21 zikizotapakaa kila sehemu ya
Taifa la Tanzania.
0 Maoni