Mmiliki wa mgodi wa
Ikombo Hill uliopo katika Kijiji cha Matonya, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma,
Bi. Doreen Kissia, ameibuka kuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya uchimbaji wa
madini ya shaba, akiwa mwanamke pekee anayeongoza mgodi unaotoa ajira kwa zaidi
ya asilimia 98 ya wakazi wa vijiji vya Matonya na Kinusi.
Bi. Doreen ameonesha
uongozi bora na ubunifu kwa kufanikisha ujenzi wa barabara ya kilomita moja
inayounganisha mgodi huo na barabara kuu, jambo lililorahisisha usafirishaji wa
madini. Kwa sasa, mgodi huo unazalisha wastani wa tani 30 za madini ya shaba
kwa mwezi.
Akizungumza katika
mahojiano maalum, Bi. Doreen ameiomba Serikali kusaidia kupeleka umeme katika
mgodi wake ili kupunguza gharama kubwa za uendeshaji zinazotokana na matumizi
ya jenereta.
Kwa upande wake,
Mhandisi Chacha Megewa wa Tume ya Madini, ametoa elimu kwa Bi. Doreen na
wachimbaji wengine kuhusu umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya uchenjuaji.
Amebainisha kuwa changamoto kubwa kwa wachimbaji wa shaba ni ukosefu wa
teknolojia hiyo, hali inayosababisha mawe yenye kiwango kidogo cha shaba (low
grade) kutupwa.
“Teknolojia ya
uchenjuaji haimaanishi lazima uwe na mtambo mkubwa. Hata kiwanda kidogo
kinaweza kuongeza thamani ya madini. Ukiweka mtambo mgodini, unapunguza pia
gharama za kusafirisha malighafi kwenda viwandani,” amesema Mhandisi Chacha.
Ameeleza kuwa kupitia
teknolojia hiyo, inawezekana kuongeza kiwango cha shaba kutoka asilimia 1 hadi
20, na kuuza madini hayo kama ‘cathode’ badala ya kuyauza kama malighafi ghafi.
Naye Mkaguzi wa
Migodi kutoka Tume ya Madini, Bw. Fahad Mkuu, amewahimiza wachimbaji
kutowahusisha watoto katika shughuli za migodini kutokana na hatari zake kwa
watoto. Pia amesisitiza umuhimu wa kuweka akiba na kutumia mapato yao kwa
maendeleo ya familia na vijiji badala ya matumizi yasiyo ya lazima.
Tume ya Madini
kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi ya Mkoa wa Dodoma, kwa kushirikiana na
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), inaendelea kutoa mafunzo kwa
wachimbaji wadogo wa madini ya kimkakati kama shaba kupitia mradi wa kuendeleza
madini yaliyosahaulika. Mradi huu umetajwa kuwa mkombozi kwa kuwapatia
wachimbaji elimu, ushauri wa kitaalamu, na mbinu za kukabiliana na changamoto
mbalimbali katika Sekta ya Madini.
0 Maoni