WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ameutaka uongozi wa Shirika la Viwango Tanzania kutokuwa na huruma na
bidhaa zisizokuwa na ubora kwani Serikali inataka soko la Tanzania liwe na
bidhaa bora, salama na zenye kuleta tija kwa mlaji na kwa uchumi.
Amewataka wazalishaji
wa bidhaa na huduma, wahakikishe wanazingatia taratibu za vipimo, uthibitishaji
wa ubora, na uboreshaji wa mifumo ya uzalishaji. “Muhakikishe bidhaa zenu
zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa vilivyowekwa na TBS”.
Ametoa maagizo hayo
leo (Jumatano, Juni 4, 2025) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jingo
la maabara na ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika eneo la
Njedengwa jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kufuatwa kwa viwango vya ubora.
Waziri Mkuu ametoa
wito kwa wafanyabiashara na waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, wana wajibu
wa kuhakikisha bidhaa wanazoingiza nchini ni salama, zimeidhinishwa na zina
alama ya ubora kutoka TBS au taasisi zinazotambulika.
“…Msikubali kubeba lawama ya kuruhusu bidhaa
isiyokuwa na ubora halafu ikaua Watanzania, haifa haifai peleka kuiteketekeza
na tunauhakika na maabara zetu. Tanzania sio shimo la bidhaa zisizokuwa na
ubora.”
Amesema Serikali ya
Awamu ya Sita inatambua kuwa viwango vya ubora si tu vinahusiana na bidhaa
bora, bali vinaimarisha afya na uchumi imara wa nchi. “Viwanda vyetu vinapaswa
kuzalisha bidhaa ambazo zinaweza kununulika hata nje ya nchi, tunataka mataifa
mengine yakimbilie bidhaa zetu.”
Amesema mradi huo
unakwenda sambamba na juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya afya kupitia
usimamizi wa ubora wa bidhaa, vifaa tiba, vyakula, vipodozi na kemikali
mbalimbali. “TBS ni mlinzi wa viwango; na kwa miundombinu hii mipya, huduma
zitaimarika na kuchangia kulinda afya za wananchi.”
Kwa upande wake,
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Jafo ametumia fursa hiyo kumshukuru
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na miongozo yake ya
kuhakikisha Taifa linazidi kupata maendeleo.
Akizungumzia kuhusu
viwango vya ubora wa bidhaa, Dkt. Jafo amesema Serikali inataka kuhakikisha
viwango vinazingatiwa na wanataka nchi iendelee kuheshimika kwa upande wa
viwango na maabara inayojengwa ni kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na
Kati.
Naye, Mkurugenzi Mkuu
wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amesema lengo la kujenga jingo hilo ni pamoja na
kusogeza huduma za viwango karibu na wananchi hasa wa Kanda ya Kati, kupunguza
utegemezi wa maabara za Dar es Salaam na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa
ubora wa bidhaa na huduma.
Dkt. Ashura amesema
kuwa ujenzi huo ambao umefikia asilimia 76 unatarajiwa kukamilika Agost, 2025
na utagharimu shilingi bilioni 25.3. Kukamilika kwa ujenzi wa jingo hilo
kutapunguza msongamano wa sampuli za bidhaa mbalimbali katika maabara
za Dar es Salaam.
0 Maoni