Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Tanzania inatarajia kuzalisha umeme unaotokana na nyuklia utakaojumuishwa katika Gridi ya Taifa ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme yanayotokana na ongezeko la viwanda.
Dkt. Biteko amesema
hayo Juni 30, 2025 Kigali nchini Rwanda wakati akihutubia katika Mkutano kuhusu
masuala ya Nyuklia Afrika.
“Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kupitia uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
imeiagiza Wizara ya Nishati chini ya uongozi wangu kuhakikisha kwamba hivi
karibuni umeme utakayozalishwa unajumuishwa katika Gridi ya Taifa,” amesema
Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa
kupitia agizo hilo Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo
kuandaa mikakati ya pamoja ya taasisi za Serikali ili kufikia azma ya kuzalisha
umeme wa nyuklia kwa kuwa ni nishati yenye unafuu wa gharama kulinganisha na
vyanzo vingine vya nishati, pia isiyochafuzi kwa mazingira.
Ametaja baadhi ya
jitihada kuwa Juni 2025 Tanzania iliandaa warsha ili kutoa uelewa kwa wadau wa
masuala ya nyuklia ikiwa ni pamoja na kuanzisha taasisi itakayoratibu na
kusimamia shughuli za nyuklia.
“Serikali yangu
itahakikisha inaendeleza mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa nishati
kwa kutumia nyuklia kwa kutunga sera thabiti na kuanzisha mifumo ya sheria na udhibiti kwa ajili ya usimamizi wa
raslimali ya nyuklia na uzalishaji wa umeme unaotokana na nyuklia, amesisitiza
Dkt. Biteko.
Vilevile amesema
Serikali itaongeza raslimali watu wenye ujuzi katika teknolojia za nyuklia ili
kutumia kikamilifu raslimali hiyo hususan katika maeneo mengine ikiwemo afya na
kilimo.
Amesema tayari
Tanzania ina nyaraka mbalimbali zinazoiangazia nyuklia kama raslimali ya msingi
kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya nishati ya baadae kama vile Sera ya Taifa ya
Nishati, Mkakati wa Nishati Jadidifu na Sera ya Maendeleo ya Madini.
Hata hivyo amesema
Serikali ina lengo la kuimarisha Sera ya Teknolojia ya Nyuklia ya mwaka 2013
ili kiakisi maendeleo ya hivi karibuni sambamba na kufuata viwango vya
kimataifa.
Akifungua Mkutano huo
Waziri Mkuu wa Rwanda Mhe. Dkt. Edward Ngirente amesema kuwa ili kufikia Mpango
wa Maendeleo wa Rwanda wa mwaka 2050 wa kuwa nchi ya kipato cha juu wanahitaji
kuwa na uzalishaji wa umeme kwa kiasi kikubwa.
“ Hivyo, Rwanda
tumeamua kuzalisha umeme wa nyuklia kwa kuwa ni salama na wa uhakika na
hauhitaji mvua ili kurahisisha
maendeleo kwa kutumia teknolojia,” amesema Mhe. Ngirente.
Aidha, amesema
Mkutano huo wa nyuklia utakuwa na manufaa kwa Afrika katika kusaidia maendeleo.
Pia nchi za Afrika kwa pamoja lazima
ziwe kinara katika matumizi ya nishati safi na kuwa muda wa utekelezaji
ni sasa ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na ongezeko la idadi ya watu.
Waziri Mkuu wa Niger,
Mhe. Ali Mahamane Lamine Zeine amesema kuwa nchi yake ina vyanzo vingi vya
nishati ikiwemo maji na sasa imezindua mpango wake wa nyuklia hivyo nyuklia ni
nishati safi na ina manufaa makubwa katika uzalishaji wa umeme barani Afrika.
Naye, Mwenyekiti wa
Bodi ya Mionzi ya Atomiki Rwanda, Dkt. Lassina Zerbo amesema kuwa Rwanda ipo
katika hatua za mwishoni za kuanzisha vinu vya nyuklia vya kuzalisha umeme.
Ameongeza kuwa katika
kufikia hatua hiyo ilihitaji dhamira ya viongozi na imani kwa wananchi juu ya
umuhimu wa uzalishaji wa umeme wa nyuklia.
Mkutano huo
unaofanyika kuanza Juni 30 hadi Julai 1, 2025 nchini humo unajumuisha wadau wa
nishati kutoka ndani na nje ya Afrika wenye lengo la kuharakisha matumizi ya
nyuklia kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuleta mabadiliko ya
nishati Afrika.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza na Washiriki mbalimbali wa Mkutano unaohusu masuala ya Nyuklia Afrika uliofanyika Juni 30, 2025 Kigali nchini Rwanda.
Baadhi ya Washiriki
mbalimbali wa Mkutano unaohusu masuala ya Nyuklia Barani Afrika wenye lengo la
kuharakisha matumizi ya nyuklia kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuleta mabadiliko
ya nishati Afrika ulioanza leo Juni 30, 2025 Kigali nchini Rwanda.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akisalimiana na Waziri Mkuu wa Rwanda, Mhe. Dkt. Edouard Ngirente wakati alipowasili katika Mkutano unaohusu masuala ya Nyuklia Afrika uliofanyika Juni 30, 2025 Kigali nchini Rwanda.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni