Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa nchi za Afrika kupewa
uhuru wa kuzalisha nishati kwa kutumia rasilimali zilizopo barani humo.
Dkt. Biteko ametoa
wito huo leo Juni 19, 2025 wakati akizungumza katika Jukwaa la Kimataifa la
Uchumi la St. Petersburg linalofanyika nchini Urusi.
Amesema Afrika
inahitaji programu itakayosaidia kufikia dhamira yake ya kuondoa idadi kubwa ya
watu ambao hawatumii nishati safi huku akitaja baadhi ya athari za matumizi ya
nishati isiyo safi ikiwemo uharibifu wa mazingira.
Ameongeza kuwa Afrika
ina vyanzo vingi vya kuzalisha nishati,
mfano Tanzania kuna vyanzo kama vile jua, maji na gesi asilia. Hata hivyo
barani humo hakuna uhuru wa kutumia makaa ya mawe licha ya kuwepo kwa kiwango
kikubwa pamoja na kuwa nchi kubwa duniani zinaweza kufanya hivyo.
“ Hivyo iangaliwe
namna kwa kila nchi kutumia rasilimali zake ili kuzalisha nishati, mfumo uliopo
unazifanya nchi zote kuwa sawa lakini ukweli ni kwamba hatuko sawa. Kwa mfano
Afrika inachangia asilimia 3 hadi 4 pekee ya uchafuzi wa mazingira, lakini
imepewa mzigo mkubwa zaidi,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza” Kila
nchi itumie utaratibu wake wa kuzalisha nishati lakini kwa lengo la kupunguza
uchafuzi wa mazingira.”
Amezungumzia
uhusiano mzuri uliopo wa kidiplomasia
kati ya Tanzania na Urusi na kusema kuwa uendelee kuwa wa kuheshimiana na
kukubaliana.
Ambapo ametaja
manufaa yake kuwa ni pamoja na
kubadilishana ujuzi na kuisaidia Tanzania katika mitaji ya miradi nishati.
Amebainisha kuwa
Tanzania ina mpango wa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha takribani
megawati 120 za umeme.
Kwa upande wake,
Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev amesema kuwa Rais wa nchi hiyo
Mhe. Vladimir Putin amekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha zinaungana na
nchi zingine katika kupatia ufumbuzi changamoto
za masuala ya nishati.
Naye, Mwenyekiti
Mtendaji wa Kampuni ya African Energy Chamber, Bw. NJ Ayuk amesema kuwa ni
muhimu kwa nchi za Afrika na Urusi kuungana na kuhakikisha sauti ya Afrika
inasikika na kutekeleza wanayokubaliana ili wote waweze kunufaika na uhusiano
kati yao.
Aidha, ameiomba
Serikali ya Urusi kuwezesha kampuni kutoka nchini humo ili ziweze kuwekeza
zaidi Afrika hususan katika sekta ya nishati.
Pia, ameipongeza
Tanzania katika hatua iliyopiga na mafanikio yake katika sekta ya nishati sambamba na kutoa wito kwa nchi za Afrika
kujifunza zaidi kutokana na mafanikio yaliyopo nchini Urusi.
Jukwaa hilo la
Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg linatarajiwa kuwa na washiriki kutoka
takribani nchi 140.
Na. Ofisi ya Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni