SERIKALI imetoa Hati za Makosa kwa Kampuni 95 za Uchimbaji Mkubwa na wa Kati wa Madini
kutokana na wamiliki wa leseni hizo kukiuka masharti ya Leseni kama yalivyoainishwa kwenye Sheria ya Madini.
Akizungumza leo Mei 6, 2025 jijiini Dar es Salaam, Waziri wa
Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kampuni hizo zinapaswa kujibu hoja ndani
ya siku 30 la sivyo zitafutiwa leseni zao.
Hati hizo za makosa zimetolewa rasmi kuanzia Aprili 14, 2025
na muda wake utamalizika Mei 13 mwaka huu.
“Kama wanahoja walete
majibu yao, tuyahakiki tukijiridhisha na hoja zao tutawaondolea makatazo kama
hawana hoja tutawafutia leseni zao kwa
mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123
ya utoaji na ufutaji wa leseni
za madini na uchimbaji kifungu cha 63 na
Kanuni zake, ambacho kinaeleza ukipewa leseni unapaswa uanze kazi ndani ya
miezi 18.”
Amesema, Serikali imetoa leseni kwa wachimbaji wa kati na
wakubwa ambazo tangu kutolewa kwake hazifanyiwa kazi.
“Zipo Kampuni tangu zimechukua leseni mwaka 2011 mpaka leo
hazijaingiza hata koleo kwenye eneo miaka 14 sasa hazijaanza shughuli zozote,
hatuwezi kuwa nchi ya namna hii,” alisema Mhe. Mavunde.
Leseni 7 tu kati ya 95 ukiziweka pembeni zina mtaji wa
Shilingi Trilioni 15 zimelala, sisi hatuwezi kuwa nchi ambayo inatoa leseni kwa
ajili ya kuchochea sekta ya madini kukua,halafu kuna watu wanachukua leseni
wanakaa nazo hawafanyii kazi kwa kisingizio kuwa tupo kwenye mazungumzo na
serikali na sababu mbali mbali.
Leseni za madini zikitolewa zina masharti nyuma yake kwenye
ile karatasi hakuna sharti linalosema mtu ataanza uchimbaji wa madini nchini
Tanzania akikamilisha mazungumzo na serikali, hiyo si sehemu ya sharti.
Masharti ni kwamba mwombaji anapopewa leseni ni lazima aanze
uchimbaji ndani ya miezi 18 vinginevyo awe na sababu ambazo zimeridhiwa na
Waziri wa Madini kupitia Tume ya Madini, vinginevyo unapaswa kuanza uchimbaji
ndani ya miezi 18.
Amesema na wale wote ambao wamepata hati ya makosa ambao wamejibu waende na barua ya
‘Commitment’ ya kueleza wataanza uchimbaji lini, ambao katika barua hiyo pia
ikitokea ameshindwa kukidhi kile alichosema kwenye barua sheria itafuata mkondo wake.
Kuna vitu kama nchi ni lazima tuchukue maamuzi magumu,
hatuwezi kuifanya nchi yetu mtu anakuja anachukua leseni alafu akaitafutie
mtaji, sheria inataka mtu yoyote anayekuja kufanya maombi ya leseni lazima atoe
udhibitisho wa uwezo wa kifedha na kiufundi kabla ya kupata leseni, sio nikupe ndio ukatafutie mtaji maana yake
utakuwa umekiuka masharti ya sheri kwa kutoa taarifa ambazo sio sahihi wakati
wa kuomba leseni.
Wale wote ambao hawatajibu ndani ya muda uliowekwa
wasitegemee huruma yoyote, na wamekuwa ni mabingwa wakukimbilia mahakamani
kuishtaki serikali katika hili Serikali imefuata taratibu zote kwa mujibu wa
sheria inayowataka waliopata Leseni wote kufanya uendelezaji wa Leseni zao,” alisema
Mhe. Mavunde.
Sekta ya Madini ni kati ya sekta zenye mchango mkubwa katika
kukuza uchumi wa nchi hivyo shughuli za uchimbaji wa madini huchochea maendeleo
makubwa ya kiuchumi.
0 Maoni