WANANCHI
wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kuacha uvivu na badala yake wachangamkie fursa
zilizopo kwenye sekta ya madini hususani
katika mgodi wa kati wa Elianje uliopo
kitongoji cha Namungo, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Rai
hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kijiji
cha Chingumbwa, kilichopo Kata ya
Namungo, Abdallah Rashid akielezea fursa zilizopo mkoani humo kupitia Sekta ya
Madini.
“Fursa
zipo nyingi ni uvivu tu wa wananchi wetu, ukiangalia kwenye mgodi huu
unaotuzunguka wa Elianje Genesis kuna fursa ya usambazaji vyakula, vinywaji,
usafi, kupika, kusambaza vifaa vya usalama migodini, uchimbaji na uchenjuaji
lakini ndio hivyo,”amesema Abdallah.
Aidha,
Mwenyekiti huyo amesema uwepo wa mgodi huo umetoa manufaa makubwa kwa wananchi
kwa kuchimbiwa kisima cha maji ambacho kwa sasa kinahudumia kaya 918, awali
kulikuwa na shida ya maji na wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu
kuchota maji.
“Pia,
mwekezaji ametujengea shule ambayo kwa sasa ina wanafunzi 79, awali watoto
walitembea umbali mrefu zaidi ya kilomita tatu kufuata shule vijiji vya jirani
hali iliyopelekea baadhi yao kuacha shule. Pia mwekezaji amekua akitoa chakula
kwa wanafunzi kipindi cha mitihani, kuwaletea vifaa vya michezo vya mpira wa miguu kwa wanaume na netball kwa wanawake na yupo mbioni kununua basi la
shule,” amesema.
Kwa
upande wa Mkuu wa Shule ya Msingi Chingumbwa iliyopo kata ya Mbekenyela mkoani
humo, Joseph Raymond amesema mgodi wa Elianje umejenga ofisi za Walimu,
kuwawekea umeme kwa ajili ya kambi kwa
darasa la saba na la nne itakayoanza mwenzi ujao wa sita wakijiandaa na mitihani ya taifa.
Naye,
Meneja wa Mgodi wa Elianje, Philibert Masawe akizungumzia mgodi huo amesema
wanajishughulisha na uchenjuaji wa
madini ya dhahabu na uchimbaji wa ‘green garnet’.
Amesisitiza
pia Kampuni ya Elianje imejenga kituo
cha mfano cha uchenjuaji wa madini ya dhahabu kinachotumia teknolojia ya CIP
ambacho kina uwezo wa wa kuchenjua mbale (mwamba) ya dhahabu kiasi cha tani 500
kwa siku.
Amesema
pia kiwanda hicho kimeajiri watanzania 300 na kuipongeza Serikali kuweka sera
rafiki na sheria nzuri ambazo zinavutia uwekezaji.
0 Maoni