Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden umeratibu ushiriki wa
ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Mazingira duniani unaofanyika
tarehe kuanzia leo tarehe 7 hadi 8 Mei, 2025, jijini Copenhagen nchini Denmark.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Masauni,
ambapo mawaziri 30 wanaosimamia masuala ya mazingira kutoka katika mataifa
mbalimbali, Kamisheni ya Umoja ya Ulaya na wadau wengine wa mazingira
wameshiriki.
Lengo la mkutano huo ni kupokea taarifa ya kila nchi ya
namna ilivyochangia katika kupunguza gesi joto duniani, kubadilishana uzoefu na
kuweka mipango ya maandalizi ya mkutano wa COP 30 unaotarajiwa kufanyika mwezi
Novemba, 2025 nchini Brazil.
Ajenda ya Tanzania katika mkutano huo ni kuongeza
upatikanaji wa fedha katika utekelezaji wa programu za mabadiliko ya tabianchi,
nishati safi ya kupikia na kuhakikisha kuwa fedha zilizokuwa zimeahidiwa na
wafadhili mbalimbali kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi hiyo zinatolewa kwa wakati.
Ajenda nyingine ni kushawishi wadau wa mazingira kutoa
misaada yenye masharti nafuu ya kutekeleza programu za mazingira na kuwekeza
katika teknolojia ya upimaji wa hewa ya kaboni ikiwa ni pamoja na kujengea
uwezo taasisi zinazoratibu masuala ya mazingira nchini.
Kwa upande mwingine, Tanzania imeeleza nia yake ya kuendelea
kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali kwa njia ya ubia na kwa kutumia rasilimali zake za asili
kama vile bahari, misitu, madini adimu, maziwa, mito pamoja na ujenzi wa miundombinu rafiki kwa mazingira.
Copenhagen, 07/05/2025.
0 Maoni