Tanzania imepiga hatua katika viwango vya kimataifa vya Uhuru wa Vyombo vya Habari, kwa kupanda kutoka nafasi ya 97 mwaka 2024 hadi nafasi ya 95 mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka
(Reporters Without Borders – RSF) iliyotolewa tarehe 2 Mei 2025, licha ya
Tanzania kupanda kwa nafasi mbili, alama za jumla zimepungua kidogo kutoka
54.80 mwaka 2024 hadi 53.68 mwaka huu.
Ripoti hiyo inayotolewa kiila mwaka imeonesha kuwa Kupanda
kwa nafasi ya Tanzania kunahusishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na
Serikali pamoja na wadau wa sekta ya habari katika kuboresha mazingira ya kazi
kwa waandishi wa habari na kukuza uhuru wa vyombo vya habari.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na mapitio ya sheria
zinazohusiana na habari, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016,
ambapo maboresho yamelenga kuondoa vifungu kandamizi na kuweka mazingira
wezeshi kwa wanahabari.
Aidha, hatua nyingine zilizosaidia kupanda ni pamoja na
kuimarika kwa mawasiliano kati ya Serikali na vyombo vya habari kupitia
majukwaa ya majadiliano ya wazi kumesaidia kujenga uaminifu na kuongeza uwazi
katika upatikanaji wa taarifa.
Vilevile, Serikali imeonyesha dhamira ya kulinda haki za
msingi kwa raia, ikiwemo haki ya kupata taarifa na uhuru wa kujieleza, hatua
iliyosaidia kuboresha taswira ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa.
Ripoti ya RSF hutathmini hali ya uhuru wa vyombo vya habari katika nchi 180 kwa kutumia vigezo vitano vikuu ambavyo ni kisiasa, mfumo wa kisheria, mazingira ya kiuchumi, mazingira ya kijamii na usalama wa waandishi wa habari.
Na. Mwandishi Wetu- JAB
0 Maoni