Serikali ipo mbioni kutambulisha Leseni mpya ya uzalishaji
wa chumvi ili kuiondoa chumvi katika kundi la madini mengine na hivyo kuchochea
ukuaji wa tasnia ya uzalishaji chumvi nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma wakati wa Kikao cha Waziri
wa Madini Mh. Anthony Mavunde na Uongozi wa Chama cha Wazalisha Chumvi Tanzania
(TASPA), kikao ambacho kimelenga kuboresha sekta ya madini kupitia tasnia ya
chumvi.
“ Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan ametupa maelekezo mahsusi
kuwezesha wachimbaji wa madini na wazalishaji wa madini chumvi nchini ili kuchochea
ukuaji wa sekta ya madini.”
Serikali imesikia kilio chenu cha muda mrefu cha uwepo wa
Leseni moja ya uzalishaji wa Chumvi ambayo itasaidia kumuendeleza mzalishaji
chumvi kwa kupunguza gharama za uzalishaji na kuyaondoa madini chumvi katika
kundi la madini mengine.
Naelekeza kuanza mara moja mchakato wa mabadiliko ya sheria
ili kuruhusu uanzishwaji wa Leseni maalum ya uzalishaji chumvi ambayo pia tozo
yake kwa hekta iangaliwe upya kufikia 20,000 kutoka kiwango kilichopo sasa.
Dhamira ya serikali ni kuona wazalishaji wa chumvi
wanaongeza tija na kufikia hatua ya kumiliki viwanda vya uchakataji na
usafishaji chumvi nchini ili chumvi yetu iwe yenye ubora na shindani,” alisema
Mavunde.
Aidha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Eng. Yahaya Samamba
ameipongeza TASPA kwa kazi ya kuwaendeleza na kuwasimamia wazalishaji chumvi na
kuahidi ushirikiano wa kutosha kutoka Wizarani katika utatuzi wa changamoto za
wanachama wake.
Akitoa maelezo yake,Mwenyekiti wa TASPA Bi. Hawa Ghasia ameipongeza wizara ya madini kwa utaratibu wa kuwasikiliza wadau na kutafuta suluhisho ya changamoto zao na kutumia fursa hiyo kumpongeza kipekee Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kusikia kilio cha wazalishaji wa chumvi kwa kujenga kiwanda cha Kuchakata na kusafisha chumvi kinachojengwa mkoani Lindi na Shirika la Madini la Taifa(STAMICO).
0 Maoni