Serikali imethibitisha kuwa inaendelea
na hatua za awali kuelekea ujenzi wa daraja la kudumu linalounganisha Kijiji
cha Negero katika Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, ili kuboresha miundombinu na
kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la
Kilindi, Mhe. Omar Mohamed Kigua, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI,
Mhe. Zainab Katimba, amesema serikali tayari imeshakamilisha usanifu wa daraja
hilo, ambao uligharimu shilingi milioni 70 na kukamilika mwezi Machi 2025.
“Serikali inatambua umuhimu wa daraja
hili kwa maendeleo ya wananchi wa Kijiji cha Negero. Hivi sasa tupo kwenye
hatua ya kupitia taarifa ya usanifu ili kupata gharama halisi za ujenzi. Baada
ya hatua hiyo kukamilika, daraja litaombewa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi
wake,” alisema Mhe. Katimba wakati akihutubia Bunge Jijini Dodoma.
Kwa sasa, wananchi wa eneo hilo
wanategemea kivuko cha chuma kwa waenda kwa miguu (Pedestrian Suspension
Bridge) chenye urefu wa mita 100, kilichojengwa na kukamilika mwezi Desemba
2021 kwa gharama ya shilingi milioni 66.68, ili kuwasaidia kuvuka Mto Negero
kwa urahisi.
Mhe. Katimba aliongeza kuwa Serikali
itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja hususan katika maeneo
ya vijijini ili kurahisisha usafiri na kuongeza fursa za
kiuchumi kwa wananchi.
Na. OR-TAMISEMI
0 Maoni