Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema Serikali itaendelea kuiamini na kukiunga Mkono Chama cha Msalaba
mwekundu (RED CROSS) ili kiendelee kufanya kazi yake nzuri ya kuwahudumia
Watanzania.
Dkt. Biteko amesema hayo Mei 10, 2025 Jijini Dodoma wakati
akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika maadhimisho ya miaka 63 ya Chama cha Msalaba Mwekundu (RED
CROSS).
Amewahimiza viongozi na wanachama wa chama hicho kutembea
kifua mbele na kijisimamia na kujipambanua kutokana na kazi nzuri wanayoifanya
bila kujali hali wala mazingira ya kazi husika.
Amesema Serikali tayari kuendelea kufanya kazi na Chama cha
Msalaba mwekundu ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata huduma bora
ikiwemo masuala ya uokoaji maisha.
“Serikali inatambua kazi inayofanywa na Chama cha Msalaba
mwekundu kupitia Ofisi na matawi yake nchi nzima,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kazi zinazofanywa na Chama cha Msalaba mwekundu
katika masuala ya kibinadamu zinaonekana ikiwemo ujenzi wa Nyumba 35 kwa ajili
ya waathirika wa mafuriko yaliyoikumba Hanang mwaka 2023.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Ajira,
Vijana na Wenye Ulemavu kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Ridhiwani
Kikwete amewapongeza Red Cross kwa kazi nzuri ya utoaji wa huduma
zinazothibitika kwa vitendo.
Amesema utendaji wao unaonesha na kufuata maono ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya
kuhamasisha utoaji huduma bora kwa Watanzania.
Naibu Waziri wa Uchukuzi ambaye pia ni Rais wa RED CROSSmhe.
David Kihenzile amepongeza juhudu za Serikali ya Muungano wa Tanzania katika
kuuga mkono juhudi za chama cha Msalaba mwekundu katika utoaji wa huduma kwa
jamii.
Pia ameishukuru Serikali kwa hatua yake kuongeza huduma kwa
jamii ikiwemo utoaji wa dawa na Vifaa tiba hatua ambayo imeendelea kuboresha
maisha ya Watanzania.
Amesema kwa sasa asilimia 30 ya watu wanaopata ajali ndio
wanaopata huduma ya kwanza kutokana na wengi kukosa elimu ya utoaji wa huduma
hiyo.
Mhe. Kihenzile pia ametumia jukwaa hilo kuhimiza jamii
kujenga moyo wa huruma na upendo na kuwajali wenye shidamiongoni mwa wanajamii
ili kujenga taifa lenye maendeleo na ustawi endelevu.
Amesema RED CROSS itaendelea kuungana na Serikali kutoa
huduma kwa Wananchi watakaopata majanga ma mahitaji ya aina mbalimbali
yanayoweza kutatuliwa kwa msaada wa kibinadamu.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 63 ya Red Cross mwaka 2025
ni Kudumisha Ubinadamu.
0 Maoni