Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya umeme
huku akisisitiza kuwa ni lazima
Watanzania wapate huduma ya umeme.
“ Tunamshukuru Mhe. Rais ambaye anasema wananchi wapate
umeme, Naomba nikuahidi Mhe. Rais mimi na wenzangu tutafanya kazi kwa kasi
unayohitaji ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amesema hayo Mei 2, 2025 wilayani Urambo, mkoani
Tabora mara baada ya kukikagua Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha
Msongo wa Kilovoti 132/33.
Dkt. Biteko amelipongeza na kulishukuru Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) kwa kukamilisha mradi kwa ufanisi “Mmefanya kazi kwa
vitendo, nilikuja hapa mwaka jana mradi ukiwa asilimia 10, maajabu gani
mmefanya mmemaliza kazi kwa wakati siwezi kujua. Nataka niwaambie naona fahari
kuwa kiongozi wenu, napenda kufanya kazi na watu wenye kuleta matokeo
nawashukuru mno.”
Vilevile, ameipongeza Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa
Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme ( ETDCO) kwa usimamizi mzuri
wa Kituo hicho cha Urambo ambacho
kimewashwa kwa siku 20 hadi sasa na kuongeza mapato ya TANESCO kwa asilimia 10.
Ameitaka Kampuni hiyo kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na
kusema kuwa wana fursa ya kupewa mradi mwingine kwa kuwa wamefanya kazi nzuri.
Amewahakikishia wananchi wa Urambo na Kaliua kuwa
wataendelea kupata umeme wa uhakika na mradi huo unaifanya Tabora kuwa chanzo
cha umeme katika mikoa ya Katavi na Kigoma.
Amesisitiza “ Mwisho wa
mwezi huu wa tano tutazima jenereta Mpanda na kusaidia wao wapate umeme, watu wa Urambo nataka
niwaambie kabla ya Kituo hiki kuwashwa makusanyo ya TANESCO yalikuwa milioni 323
pekee na baada ya kuwashwa Wilaya ya Urambo inaweza kuipatia TANESCO kwa mwaka
shilingi bilioni 4.5 kiuchumi maana yake tumewekeza shilingi bilioni 44 na hiyo
fedha itarudi ndani ya muda mfupi,”
Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amempongeza Mbunge wa Urambo,
Mhe. Margaret Sitta kwa mchango wake na ufuatiliaji wa ujenzi wa mradi wa Kituo
hicho na kusema kuwa alijitoa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya
umeme.
Aidha, amesema sekta ya nishati imenufaika na mchango wake
na kuielekeza TANESCO kupanda mti na kuupa ukumbi wa mikutano jina la Mbunge
huyo ikiwa ni sehemu ya kuthamini na kuenzi mchango wake.
Pia, ameielekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupeleka
umeme katika vitongoji huku Urambo ikipewa kipaumbele.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, amewasihi Watanzania kushindana kwa hoja na
sera, huku akiwaomba wamuunge mkono Rais Samia kwa nia yake thabiti ya
kuwaletea maendeleo wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Urambo, Mhe. Margaret Sitta amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 wamepata fedha zaidi ya
shilingi bilioni 100 ambapo barabara imetumia shilingi bilioni 12, sekta ya
elimu imetumia shilingi bilioni 25 pia wana shilingi bilioni 7 kwa ajili ya
ujenzi wa matanki ya maji huku wakisubiri mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria.
Kuhusu umeme, Mhe. Sitta amesema awali wananchi walikuwa wakichanga fedha kwa ajili ya
kununua jenereta lakini sasa wanaishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya
ujenzi wa mradi wa umeme.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba
amesema kufuatia maelekezo na usimamizi makini wa Dkt. Biteko sasa wananchi
wanapata umeme wa uhakika.
“ Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ni vyema ukafahamu kuwa tangu
umeme huu ulivyowashwa haujawahi kuzimika hata mara moja na haya ni matokeo ya
usimamizi wako na nina amini wananchi hawa wa Urambo leo wana haki ya kufurahia
uwepo wako,” amesema Mhandisi Mramba.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), CPA Renata Ndege amesema mradi huo una km 135 kutoka Tabora hadi
Urambo ambao unasaidia kuufungua Mkoa huo na mikoa jirani kwa fursa za kiuchumi
na kijamii.
“ Mradi huu umekamilika na tumewasha umeme Machi 20, 2025,
aidha mahitaji ya umeme kwa Mkoa wa Tabora ni wastani wa megawati 28 sawa na
asilimia 32.7 ya uwezo wa vituo vyote ambayo ni megawati 85.5,” amesema Ndege.
Amebainisha “ Tunakuhakikishia kuwa wananchi wanapata umeme
kama ambavyo umekuwa ukituelekeza na sasa umeme upo wa kutosha nchini.”
Msimamizi wa Mradi huo wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na
Kusambaza Umeme cha Msongo wa Kilovoti 132/33, Mhandisi Dalali Runyamila amesema kuwa kupitia mradi
huo uliogharimu shilingi bilioni 44 ikiwa ni pamoja na fidia kwa wananchi unazalisha umeme wa ziada megawati 25 na
hivyo wananchi wana umeme wa uhakika.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni