Siku moja baada ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kupandisha
kima cha chini cha mshahara wa watumishi wa Serikali kwa 35% Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mhe. Mohamed
Mchengerwa amemshukuru na kuwaelekeza watumishi chini ya Wizara yake kuwa
wazalendo na wabunifu ili kuinua uchumi wa nchi.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Mei 2, 2025 wakati
alipokuwa akiongea na watumishi wa Mkoa wa Arusha ambapo amesema Wizara yake
inasimamia takribani asilimia 76 ya watumishi wote hivyo njia pekee ya kuunga
mkono maono ya Mhe. Rais ni kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
" Ndugu zangu ili tuweze kutekeleza maelekezo ya Mhe
Rais wetu ni muhimu kutembea katika ndoto zake za kutaka kuwaletea watanzania
maendeleo". Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amesema kufuatia Rais kutoa ongezeko hilo la mshahara wa 35%
Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi pekee ambayo imewapatia wananchi wake ongezeko
kubwa barani Afrika.
Aidha, amewataka wataalam wa Serikali kwenye Halimashauri
zote nchini katika mabaraza ya madiwani kusukuma ajenda za maendeleo na kuonya
kwa baadhi ya watumishi wasio waadilifu kubadilika mara moja kabla
hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wa Wakurugenzi wa Halimashauri, amewataka
kuendelea kusimamia miradi iliyopo kwenye maeneo yao kwa kuzingatia miongozo na
sheria huku wakisahihisha makosa yaliyoainishwa ni Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali.
Amewataka waongeze mifumo ya kupata taarifa za ubadhilifu na
kuchukua hatua ili kuwadhibiti watumishi hao.
Amewapongeza kwa kazi nzuri ya kuongeza makusanyo na
kuendelea kuminya mianya ya upotevu huku
akiwataka kubuni vyanzo vipya.
Amewapongeza Wakuu wa Mikoa wote nchini kwa kuimarisha amani
na kukuza uchumi kwa kusimamia vema miradi mbalimbali kwenye maeneo yao na
kuwasisitiza kuendelea kufanya hivyo na kusisitiza kuwa kamwe siasa isiwe
kikwazo cha kufanya maendeleo.
Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda kwa
ubunifu wake na kumtaka asiyumbishwe na siasa.
Na. John Mapepele - TAMISEMI
0 Maoni