Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imesema mwenendo
wa urejeshaji wa mikopo yote iliyotolewa kwa vikundi vya wanawake,
wajasiliamali, watu wenye ulemavu na vijana kabla ya Aprili 2023 ni wenye
kuridhisha na Serikali imeendelea kusimamia ili kuhakikisha pesa yote
iliyokopeshwa inarejeshwa.
Hayo yamesemwa leo Mei 08, 2025 bungeni Jijini Dodoma na
Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Dkt. Festo Dugange wakati akijibu
swali la msingi la Mheshimiwa Mwantumu Haji Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka
kujua ni lini Serikali itaanza kuwapatia Mikopo Wajasiriamali Wadogo Wanawake
na Vijana.
Katika majibu yake Naibu Waziri Dkt. Dugange amesema,
Serikali ilifanya tathimini juu ya utaratibu wa mwanzo uliokuwa ukitumika kutoa
na kurejesha mikopo na ilibaini uwepo wa mianya ya kufanya vikundi kutorejesha
mikopo kwa ufanisi na kwa wakati unaotakiwa ndiyo maana serikali ilisitisha
mikopo hiyo na kuandaa kamati mpya, utaratibu na kanuni kwa ajili ya kusimamia
mikopo hiyo katika maeneo yote ya halamashauri.
“Mheshimiwa Spika, Serikali ilisitisha kwa muda utoaji wa
mikopo ya asilimia 10 katika mamlaka za serikali za mitaa Aprili 2023 kwa lengo
la kufanya maboresho. Aidha, mikopo hii ilianza kutolewa tena tarehe 01 Julai,
2024 kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa na Kanuni za Utoaji na
Usimamizi wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za mwaka 2024,”
alisema Naibu Waziri Dkt. Dugange.
Aidha aliongeza kuwa “Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2024/25, Serikali kupitia halmashauri ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 82.84 kwa vikundi 8,275 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 40.71 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake, shilingi bilioni 36.64 kwa vikundi vya vijana, na shilingi bilioni 5.48 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu,” amefafanua Mhe. Dugange.
Na. OR - TAMISEMI


0 Maoni