WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea na mikakati ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wa Mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Japan ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika mataifa hayo.
Mheshimiwa Majaliwa
amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kushiriki katika makongamano
mbalimbali ya kimataifa ambayo yamekuwa yakiwakutanisha wafanyabiashara na
wawekezaji ili kuongeza tija kubwa kwenye masuala ya biashara na uwekezaji.
Amesema hayo leo
(Jumatatu, Mei 26, 2025) alipofungua kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii
lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wafanyabiashara na wawekezaji
wa Japan katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Westin, Osaka, Japan ikiwa ni
sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika
maonersho ya World Expo Osaka 2025.
“Tumewaeleza
wafanyabaishara na wawekezaji hawa wa Japan fursa ambazo zipo nchini, hii ni
mara ya tatu tunakutana na wafanyabara na wawekezaji kutoka Japan, tayari
tumeanza kuona manufaa ya makongamano haya kutokana na kuongezeka kwa biashara
kati ya mataifa haya mawili.”
Waziri Mkuu amesema
hadi Machi 2025 jumla ya makampuni 24 kutoka Japan yamewekeza nchini Tanzania
katika miradi mbalimbali yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 42.70 nchini
na kuwawezesha jumla ya Watanzania wapatao 1,182 kupata ajira.
Mheshimiwa Majaliwa
amesema licha ya uwekezaji wa makampuni hayo, Serikali ya Tanzania imeendelea
kunufaika na ushirikiano wake na Serikali ya Japan kwa kupata misaada katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na
miundombinu.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu ameshuhudia utiaji saini wa hati sita za ushirikiano
ikiwemo ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya mafuta baina ya Serikali ya
Tanzania na Shirika la JGC la Japan, hati nyingine ni baina ya Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC) na Axcel Afrika kwa ajili ya kukuza uwekezaji nchini.
Hati nyingine
zilizosainiwa ni kati ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Axcel
Afrika kwa ajili ya kukuza uwekezaji Zanzibar, hati nyingine iliyosainiwa ni
kati ya Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) na Shirika la
Nishati la Toshiba, hati nyingine ni kati ya Shirika la Tiba la TOKUSHUKAI na
Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Hati nyingine
iliyosainiwa ni kati ya ushirikiano kati Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya
Benjamin Mkapa na Chama cha Maendeleo na Uchumi Afrika cha Japan (AFRECO).
Kwa upande wake,
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleimani Jafo amesema dhamira ya
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
uwekezaji inazindi kufunguka hivyo amewaomba Watanzania kuhakikisha
wanachangamkia fursa hizo kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na Taifa.
Amesema lengo la
Serikali la kuendelea kutafuta fursa hizo za biashara, uwekezaji na utalii ni
kukuza uchumi pamoja na kuwezesha upatikanaji wa ajira nchini, na kwamba
kipaumbele kimewekwa katika sekta za biashara, miundombinu, utalii, uchumi wa
buluu, uwekezaji kwa kuwa Japan imepiga hatua kubwa katika sekta hizo.
Dkt. Jafo amesema
kipaumbele kingine ni kutafuta wawekezaji watakaoshirikiana nao katika
kuendeleza sekta ya kilimo ili kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya
kilimo, kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya kisasa,
katika sekta ya madini ni kuoyaongezea thamani madini ya kimkakati.
Naye, Waziri wa
Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Omar Said
Shaaban amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga katika kutumia fursa
za uwekezaji zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Japan.
Waziri Shaaban
amesema tayari Serikali hiyo imeshaanza utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya
uwekezaji ikiwemo ujenzi wa mitaa ya viwanda ambapo mmoja umejengwa mtaa wa
Duga Zuze visiwani Zanzibar pamoja na eneo la Chamanangwe visiwani Pemba.
Mbali na miradi ya
ujenzi wa mitaa ya viwanda, pia Waziri Shaaban amesema Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara Zanzibar wameandaa
jarida linaloeleza fursa za uwekezaji Zanzibar ambalo limezinduliwa na Waziri
Mkuu na kugawiwa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan.
Amesema eneo jingine
ambalo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga kutafuta wawekezaji ni uchumi wa Buluu kupitia mazao ya bahari
ikiwemo usindikaji wa samaki ili kuhakikisha unafanyika kisasa zaidi kwa faida
ya wananchi na serikali.
Awali, Kamishina
Jenerali wa World Expo Osaka 2025 kwa Tanzania na Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis amesema kongamano hilo
ambalo ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya World Expo Osaka
2025 linalenga kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Japan.
Mkurugenzi huyo
alisema maeneo ambayo yamepewa kipaumbele katika kongamano hilo ni kwenye sekta
ya nishati, madini, kilimo, huduma za kibenki, utalii, uwekezaji, afya ambapo
wafanyabiashara wa Tanzania wanakutana na wafanyabiashara wa Japan kujadiliana
namna ya kushirikiana katika kukuza biashara na uwekezaji.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Rais na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kubota la Japan, Bw. Yaichi Kitao kwenye hoteli ya Westin, Osaka Japan, Mei 26, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
0 Maoni