Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kauli moja wamepitisha kwa kishindo Bajeti ya Ofisi ya Wizara kwa Mwaka wa
Fedha 2025/26 yenye takribani Shilingi bilioni 224.98 kwa ajili ya wizara na
taasisi zilizo chini yake kutekeleza majukumu yake.
Bajeti hiyo iliyopitishwa kwa uungwaji mkono mkubwa kutoka
kwa wabunge, inalenga kuendeleza utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika
Sekta ya Madini pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma na utendaji kazi wa
wizara na taasisi zake.
Awali, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akiwasilisha
Hotuba ya Mpango wa Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha
wa Serikali wa 2025/2026 leo Mei 02, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, ameeleza Bunge
kuwa kiasi hicho ni kwa ajili ya kuwezesha Wizara ya Madini na taasisi zake
kutimiza majukumu na wajibu wao.
“Mheshimiwa Spika, ili Wizara iweze kutekeleza majukumu na
malengo yaliyopangwa ikiwemo ukusanyaji wa maduhuli ya shilingi 1,405,537,268,755.00
(Trilioni 1.4) naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha makadirio ya
shilingi 224,984,150,000.00 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa
Mwaka wa Fedha 2025/2026,” ameeleza Mavunde.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mchanganuo wa bajeti hiyo,
Shilingi 124,604,788,000.00 (Bilioni 124.6) sawa na asilimia 55.38 ya bajeti
yote imetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo inalenga kuleta tija na
kuchochea ukuaji wa sekta ya madini hapa nchini.
Ameeleza kuwa, Shilingi 100,379,362,000.00 (Bilioni 100.3)
sawa na asilimia 44.62 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambapo kati ya
hizo, Shilingi 24,268,585,000.00 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi
(PE) huku Shilingi 76,110,777,000.00 ikitengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo
(OC) ya Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake.
Kupitishwa kwa bajeti hiyo kwa kauli moja kunatoa ishara ya
dhamira ya Serikali kuendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta ya madini ili
kuhakikisha inachangia kikamilifu katika uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi.
Katika hotuba yake, Waziri Mavunde ameeleza Wizara kuja na
Programu maalum ya “Mining for a Brighter Tomorrow (MBT)” inayolenga
kuhamasisha ushiriki wa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji
maalum kwenye mnyororo mzima wa shughuli za madini.
Aidha, kupitia, maono ya Vision 2030; Madini ni Maisha na
Utajiri, Wizara inalenga kuifanya sekta ya madini kuwa kichocheo cha maisha ya
Watanzania kwa kufanya utafiti kina wa jiosayansi kwa kutumia teknolojia ya
kisasa (airborne geophysical survey) ili kuongeza kanzidata ya jiololia ya nchi
sambamba na kuunganisha sekta ya madini na sekta nyingine kama za maji, ardhi,
afya, kilimo, kiuchumi n.k.
Katika eneo la Utafiti wa Kina na Teknolojia ya Kisasa,
Waziri Mavunde amesema, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini (GST) itaongeza utafiti wa jiofizikia kwa njia ya ndege hadi kufikia 34%
ya eneo la nchi ifikapo 2026, sambamba na Ujenzi wa maabara mpya ya kisasa
(State-of-the-Art Geoscientific Laboratory) Dodoma utaongeza uchunguzi wa
madini ya kisasa kama lithium, nickel, cobalt lakini pia ununuzi wa Helicopter
itakayofungwa vifaa maalum vya kisasa kwa ajili ya utafiti na vifaa vya kisasa
vinanunuliwa kuharakisha ukusanyaji wa taarifa.
Vilevile, Waziri Mavunde ameeleza mpango wa Serikali
kuendelea kuboresha mazingira kwa wachimbaji wadogo kwa kuwaunganisha na
taasisi za kifedha na mabenki ili waweze kupata mikopo na kukuza mitaji yao,
kuwapatia teknolojia za kisasa za uchimbaji na uchakataji madini, elimu na
maeneo ya uchimbaji na hivyo kuendesha shughuli zao kwa tija Zaidi.
Pia, Wizara ya Madini itaendelea na mkakati wake wa kujenga mfumo wa kidijitali kwa ajili ya kusimamia Sekta ya Madini kwa ufanisi na tija na kwa manufaa ya kiuchumi na taifa kwa ujumla.
0 Maoni