Watumishi wa umma ni taswira au sura ya Serikali hivyo
tunatakiwa tuangalie na kuzingatia namna tunavyofanya kazi na tunapotekeleza
majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa niaba ya Serikali. Kila mmoja
ana wajibu kwa kutunza taswira ya Serikali tunayoitumikia chini ya Uongozi wa
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice
Mtulo wakati anafunga mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani kwa muda wa siku tano.
Bi. Mtulo amewaeleza watumishi hao kuwa Serikali ina sheria,
taratibu na kanuni zinawapa mwongozo wa namna ya kufanya kazi kama mtumishi wa
umma ambapo katika hayo maadili ya utumishi wa umma, yanatuasa kuhusiana na
rushwa.
“Sisi ni Mawakili wa Serikali, tunaendesha mashauri yenye
maslahi mapana ya Serikali ambapo mashauri hayo yana kiwango kikubwa cha fedha
na yanahusisha watu mbalimbali ndani na nje ya nchi, hivyo Mawakili wa Serikali
tujiepushe na rushwa. Aidha, inapotokea unakutana na mazingira ya rushwa,
kimbia ili kulinda taswira ya taasisi na Serikali; heshima, utu na haiba yako
kwa jamii na watu wanaokutegemea,” amesisitiza Bi. Mtulo.
Bi. Alice Mtulo amewataka Mawakili hao kutunza siri za
Serikali kwa kuwa majukumu wanayotekeleza yanawapa nafasi ya kufahamu taarifa
mbali mbali. “Jinsi unavyotunza siri zako, una wajibu wa kutunza siri za
Serikali, tuwe waangalifu katika hili.Ukikutwa umevujisha taarifa za Serikali
utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” amefafanua Bi. Mtulo.
Aidha, amewaasa Mawakili hao kuzingatia mawasiliano na
uhusiano baina yao na viongozi, watumishi wengine na wadau wanaofanya nao kazi.
Alisisitiza kuwa na mipaka kwa kuzingatia taratibu za Ofisi ikiwemo kuwa makini
kwa yale wanayoandika na kuongea ikiwa ni pamoja na kufuata sheria, kutumia
hekima na busara, kuwa waaminifu na wasikivu kwa Serikali tunayoitumikia.
“Sipo tayari kumvumilia mtu yeyote asiyekuwa na nidhamu
kwake yeye mwenyewe, wenzake na kwa kiongozi wake.”
Vile vile, ametoa rai kwa Mawakili hao kuzingatia na kutumia
mifumo ya TEHAMA kwa kuwa Serikali imejikita kwenye matumizi ya mifumo ya
TEHAMA. Ofisi ina mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambapo kila mtumishi atapimwa
utendaji kazi wake kupitia mifumo hiyo. Alisisitiza kila mmoja anapaswa kujaza
taarifa za utekelezaji wa majukumu kupitia mifumo hiyo. “Ukitoka Mahakamani
jaza taarifa kwenye mifumo husika ili Ofisi ipate takwimu sahihi na kwa
wakati.” Aidha alisisitiza kuhusiana na dhumuni na wajibu wa kila mmoja kwa
Ofisi, wajibu kwa wafanyakazi wenzako na wajibu kwako wewe binafsi. “Kumbuka na
tafakari kuwa ulikuja Ofisini peke yako,
usifuate mikumbo na usiwe mwanaharakati. Zingatia sheria, taratibu na kanuni za
utumishi wa umma, endapo una mahitaji ya msingi wasilisha kwa mamlaka husika
kwa utaratibu uliowekwa na yatafanyiwa kazi,” amefafanua Bi. Mtulo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi hiyo, Bi. Asha Hayeshi amewaeleza Mawakili hao kuwa ni muhimu kwa Wakili wa Serikali kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na watumishi wenzake ili kurahisisha mgawanyo wa majukumu na matumizi bora ya ujuzi kwa kila mmoja wakati wa kuandaa majibu ya mashauri ya Serikali, kuchambua ushahidi kwa kina na kuhakikisha mashauri yanaendeshwa kwa ufanisi mkubwa kwa maslahi mapana ya Serikali.
0 Maoni