Waziri wa Nchi, Ofisi Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa
amezindua rasmi mafunzo ya utoaji wa Mikopo kwa Wakandarasi wanaotekeleza
Miradi iliyo chini ya TARURA inayotekelezwa na Benki ya CRDB kutokana na fedha
zilizokusanywa kwenye mauzo ya Hatifungani ya Miundombinu ya barabara za wilaya
(Samia Infrastructure Bond).
Uzinduzi huo umefanyika tarehe 10 Aprili, 2025 katika Ukumbi wa
Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa
hiyo ni hatua ya kihistoria ya kuzindua rasmi bidhaa ya kifedha itakayotolewa
na Benki ya CRDB kupitia fedha za Hatifungani ya Maendeleo ya Miundombinu
ambayo ni mahususi kuwawezesha Wakandarasi wazawa kufanikisha utekelezaji wa
Miradi ya TARURA nchini.
"Leo tunasimamia katika
ukingo wa kihistoria, leo sio uzinduzi tu wa bidhaa ya kifedha, leo ni uzinduzi
wa mapinduzi ya kweli, mapinduzi ya kiuchumi, mapinduzi ya kiutawala na ya
kifikra kwa Sekta ya Miundombinu nchini Tanzania."
"Kwa miaka mingi
tumeshuhudia Makandarasi wa ndani wakijitahidi, wakijituma kwa bidii lakini
wakikwama si kwa sababu hawana uwezo bali ni kwa sababu mazingira
hayakuwapendelea," amesema.
Mhe. Mchengerwa ameendelea
kubainisha kuwa Hatifungani ya Maendeleo ya Miundombinu ina maana kubwa katika dhamira ya Serikali ya
kuhakikisha utekelezaji wa Miradi ya barabara nchini chini ya TARURA,
Makandarasi sasa watapata suluhisho la kifedha litakalowawezesha utekelezaji wa
miradi kwa wakati, ufanisi na kwa viwango na ubora vinavyotakiwa.
Aidha, Mhe. Mchengerwa
alizindua mfumo wa kidijitali utakaotumika na Makandarasi kuombea mikopo
ujulikanao kama 'Samia Infrastructure Portal'
na kusema kuwa mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa fedha kirahisi kwa
Makandarasi pamoja na kupunguza muda na gharama ya ufuatiliaji kwani
unawawezesha kuomba huduma popote walipo.
Kwa upande wake Kaimu
Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Edward Amboka amemuahidi Mhe. Waziri kuwa
TARURA kwa kushirikiana na Benki ya CRDB wataendelea kuhakikisha Hatifungani
hiyo inatumiwa vyema na Makandarasi wazawa katika kutekelezwa miradi Kwa wakati
na kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa.
0 Maoni