Maparomoko ya maji Hululu au Vinile ambayo yanapatikana katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia Uluguru yanaendelea kupata umaarufu kuwa kivutio cha Utalii kufuatia jitihada zinazofanywa na Serikali za kuyatangaza na kuboresha miundombinu ya kiutalii.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) wakati akijibu swali la Mhe. Dkt. Christine Gabriel
Ishengoma aliyeta kujua Serikali itatangaza lini maporomoko ya Hululu (Vinile)
yaliyopo Mvomero kuwa Kivutio cha Utalii.
Mhe. Kitandula alisema kuwa
Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetekeleza
shughuli mbalimbali za kuboresha miundombinu ya kitalii na kutangaza Hifadhi
hiyo ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa jitihada zilizochukuliwa ili kuboresha
maporomoko hayo ni pamoja na matengenezo ya mara kwa mara ya barabara yenye
urefu wa kilometa 8 kutoka Kijiji cha Kibaoni kuelekea kwenye maporomoko,
kujenga kambi ya watalii eneo la Bunduki, kujenga ngazi za kupanda kuelekea
maporomoko hayo, kutoa mafunzo kwa waongoza watalii wenyeji (Local tour guides)
pamoja na kukarabati nyumba ya kupumzikia watalii.
Aidha, Mhe. Kitandula alisema kufuatia jitihada hizo za
Serikali, idadi ya watalii imeongezeka kutoka 290 mwaka 2021 hadi kufikia
watalii 1,453 mwaka 2024.
Maporomoko ya maji Vinile yaliyopo katika safu za milima ya Uluguru yena mtiririko wa maji mengi na safi mwaka mzima, na yamesheheni wingi wa vivutio kama vile wanyama mbalimbali, ndege, miti jamii mbalimbali, maua, na miinuko ya kuvutia kwa utalii wa kupanda milima na Utalii Ikolojia.
Na. Anangisye Mwateba - Bungeni Dodoma
0 Maoni