Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewataka wananchi kutogawanywa kwa itikadi ya dini wala siasa wakati
huu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Ubunge na Udiwani kwa manufaa ya Taifa.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 23, 2025 wilayani
Monduli mkoani Arusha wakati akizungumza na wanannchi mara baada ya kuzindua
mradi wa maji katika Kijiji cha Esilalei.
“ Ninatamani kuona hatugawanyiki na mtu yoyote wala
hatuwekwi kwenye makundi ya dini wala ukabila. Nataka niwaombe wananchi wa
Monduli pendaneni na shirikianeni na uchaguzi utakapofika chaguaneni kwa haki,”
amesema Dkt. Biteko.
Amewataka wananchi wa Monduli kuutunza mradi huo wa maji wa
Esilalei “ Nawapongeza Wizara ya Maji na RUWASA kwa kusimamia mradi huu mzuri
na wa uhakika, bila shaka mtaona itakapofika Desemba mwaka huu awamu ya pili ya
mradi itakuwa imekamilika,”
Pia, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inawapenda wananchi wa Monduli na inawapongeza
kwa uchapakazi wao kwenye kilimo na ufugaji.
Aidha, amewataka wachape kazi na kuwa Rais Samia amefikisha mradi huo wa maji kwa kuwa anapenda pia mifugo yao istawi.vilevile, amesema kuwa Rais Samia amemtuma kuwahakikishia wananchi hao kuwa wafugaji nchini wanakuwa daraja la juu kama walivyo wananchi wengine.
Pia, amesema wananchi hao wanachohitaji ni Serikali tu
iwapatie nyenzo kama maji, umeme na barabara ili kufanikisha shughuli zao
ambapo tayari Rais Samia ameapa kuwapatia nyenzo hizo.
Kuhusu umeme, Dkt. Biteko amesema kuwa vijiji vyote vya
Wilaya ya Monduli vimepata umeme na katika vitongoji 236, vitongoji 72 vimepata
umeme na vilivyosalia vitapata huduma hiyo mara baada ya Uchaguzi Mkuu.
Akijibu ombi la Mbunge wa Monduli, Mhe. Freddy Lowasa “
Nguzo za umeme 20 alizoomba Mhe. Mbunge kuanzia Alhamisi hadi wiki inayokuja
tutaanza kuona watu wa hapa wanapata umeme bila masharti yoyote, katika maisha
tunapimwa kwa kazi si kwa maneno,”
Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amezungumzia Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar na kusema kuwa Muungano huo wa miaka
61 ni wa kipekee duniani kwa kuwa mataifa kadhaa
yamejaribu kuungana lakini yameshindwa.
Aidha, Tanzania imeendelea kubaki Taifa moja lenye amani.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Dkt. Steven Kiruswa
amefurahishwa kwa Wilaya hiyo kupata maji na kusema kuwa maji ni uhai, hivyo
anamshukuru Rais Samia kwa kusaidia pia mifugo kupata maji.
Mbunge wa Monduli, Mhe. Freddy Lowasa amesema kuwa kazi
aliyofanya Rais Samia wilayani humo ni kubwa kwa kuwa huduma ya maji ilikuwa changamoto kubwa kwao.
“ Kwa miaka mingi maji yamekuwa kero kubwa katika Wilaya
yetu kwa kupata mradi huu tunaomba umpelekee shukrani zetu Rais Samia,” amesema
Mhe. Lowassa.
Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Monduli, Mhandisi Naville Msaki amesema kuwa mradi huo ulisanifiwa mwaka 2021 utahudumia wananchi 8,867 na mifugo 24,000 hadi sasa umefikia asilimia 96 na hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 2.7.
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati



0 Maoni