Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa jitihada zao za kutatua
migogoro ya ardhi wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la
kuwataka viongozi kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo jana Aprili 23, 2025
wilayani Monduli, mkoani Arusha wakati akihutubia wananchi mara baada ya
kuzindua Shule Mpya ya Sekondari ya Migungani iliyopo wilayani humo.
“Naomba kuwapongeza tena uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa
kuendelea kufanya kazi nzuri sana hapa wilayani kwa maslahi mapana ya wananchi
wa Monduli. Nimejulishwa kuwa, mmefanya mengi mno ikiwemo utatuzi wa changamoto
na migogoro ya ardhi hapa wilayani. Nimejulishwa kuwa sehemu kubwa ya
changamoto hizi mmefanikiwa kuzitatua hongereni sana,” amesema Dkt. Biteko.
Ameipongeza pia kamati ya kutatua kero za wananchi
inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ikiwa na wataalamu mbalimbali ambayo imejiwekea
utaratibu wa kupokea kero kutoka kwa wananchi na kuzipatia ufumbuzi, ambapo
ameitaka pia iratibu zoezi la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi.
Akiwa shuleni hapo, Dkt. Biteko amewapongeza wananchi kwa
kujenga shule hiyo ya Sekondari Migungani na kufikia asilimia 85 ya ujenzi huku
Serikali ikichangia shilingi milioni 500.
“ Sote tunafahamu kuwa, elimu ni msingi mkubwa wa maendeleo.
Sisi wana Monduli tayari tunayo shule yetu hii ambayo imeshakamilika. Hii ni
miongoni mwa shule zilizopo Wilayani hapa ambazo zitaendelea kutupatia elimu
kwa vijana wetu,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuwa na
wananfunzi 400 na hivyo amewataka wanafunzi kutunza miundombinu sambamba na
kujifunza kwa bidi ili wajiandae kuwa wazalendo na raia wema huku wakiwa na
uwezo wa kutafuta majibu ya matatizo watakayokumbana nayo.
Kuhusu miradi ya umeme wilayani humo, amesema kuwa mwaka huu
Serikali inatarajia kujenga mradi mkubwa wa umeme kwa lengo la kuuongezea nguvu
umeme unaopatikana ili uweze kufika Loliondo na kusaidia wilaya hiyo kuwa na umeme wa uhakika.
Aidha, Dkt. Biteko amezungumzia maadhimisho ya miaka 61 ya
Muungano kwa kuwataka Watanzania kuenzi muungano huo kwa kujenga Taifa moja kwa
kushikamana na kufanyakazi kwa pamoja
kwa kushirikiana.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Festo Kiswaga amesema
kuwa Wilaya hiyo ni tegemeo kwa Chama Cha Mapinduzi na wamekuwa wakishirikiana
na wananchi katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.
Pia, amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili
ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara, hospitali, shule na kuwa
Wilaya hiyo ni kati ya wilaya zinazofanya vizuri katika elimu na huku
akimshukuru Rais Samia kwa kuwekeza katika elimu nchini.
0 Maoni