Katibu Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amehitimisha
ziara yake ya siku tano mkoani Ruvuma, akisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa
chama cha wanachama, kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote na kuwa mtetezi wa wanyonge.
Balozi
Nchimbi amesema kwamba katika kuendeleza nafasi yake kama taasisi imara
inayohusika na uongozi wa nchi, CCM hakina budi kuendeleza misingi ya sera zake
zinazolenga kubadilisha hali za maisha ya watu, kuendana na mahitaji ya
nyakati, na kuzingatia maslahi ya taifa.
Dkt. Nchimbi
aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanaCCM na wananchi wa mji wa Songea,
waliokusanyika kumpokea alipofika kufungua mradi wa kitega uchumi wa Tawi la
CCM la Mshangano mjini Songea, Jumapili tarehe 6 Aprili 2025, ikiwa ni siku ya
tano tangu alipoanza ziara hiyo tarehe 2 Aprili 2025.
Katika ziara
hiyo aliyoanzia katika Wilaya ya Tunduru, Namtumbo, Nyasa, na hatimaye Songea
mjini, Balozi Nchimbi alitoa pongezi kwa Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia
ni Mwenyekiti wa CCM, kwa jinsi inavyotafsiri kwa vitendo na ufanisi, Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, kupitia miradi ya maendeleo na huduma kwa
wananchi.
Balozi
Nchimbi alitoa maelekezo kwa Serikali kuendelea kusimamia na kubuni mipango
inayolenga kuongeza matokeo chanya kwenye shughuli za uzalishaji mali, ikiwemo
kilimo na madini, ili wakulima na wachimbaji madini waendelee kuzalisha kwa
tija itakayoongeza pato la taifa na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, Balozi
Nchimbi alitembelea na kutoa maelekezo mahsusi katika miradi kadhaa ya
maendeleo na ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kupitia wizara na taasisi
zake, ikiwemo mradi wa uzalishaji mbegu chini ya Mamlaka ya Mbegu Nchini (ASA)
na ujenzi wa Bandari ya Nyasa, kwa lengo la kuendelea kutafsiri utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Katika
mikutano ya hadhara katika wilaya mbalimbali, pamoja na kusalimia wananchi
katika maeneo ya Songea Vijijini, Mbinga na Songea mjini, Balozi Nchimbi
alipokea taarifa za utendaji wa kazi kutoka kwa viongozi wa Chama na Serikali,
na pia alipokea maoni ya wananchi kuhusu changamoto zinazowakabili, kupitia kwa
wabunge na wananchi moja kwa moja, kisha kutoa maelekezo ya kutatuliwa kwa kero
hizo.
Balozi
Nchimbi, ambaye amehitimisha rasmi ziara yake kwa kuondoka mkoani humo Jumatatu
tarehe 7 Aprili 2025, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wanaCCM na Watanzania
wote kwa ujumla kwa ushirikiano wao na Serikali ya CCM katika kulinda tunu za
taifa, ikiwemo amani na utulivu. Alitoa wito wa kuendeleza hali hiyo wakati
nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
0 Maoni