Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
wamekutana na baadhi ya viongozi na wajumbe wa Tanzania Bloggers Network (TBN)
kwa mahojiano maalum yenye lengo chanya la kukusanya maoni yao ili kuimarisha
masuala ya blogging, nchini.
Hatua hiyo ya kukusanya maoni imekuja kufuatia wataalamu hao
kuagizwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ipo katika utafiti
maalum kwa nia ya dhati kuboresha Sera na kanuni zake mbalimbali katika eneo
hilo la majukwaa ya mtandaoni.
Kikao hicho kimefanyika kwa mafanikio katika ofisi za TBN
zilizopo kwa Aziz Ali, Temeke, watafiti hao wamechukua maoni ya TBN Makao
Makuu, wakisema pia watafika katika Ofisi za Kanda za TBN.
Akizungumza Katibu Mkuu wa TBN Khadija Kalili amesema TCRA
imefanya uamuzi sahihi kukutana na wadau wake kwa kupitia wataalamu hao kwani
maoni yao yatawapa picha halisi juu ya tasnia ya habari na blogging kwa ujumla
wake.
Amesema kilio kikubwa cha wana TBN ni gharama za usajili na
tozo ya leseni kiasi ni kikubwa ambacho kwa uhalisia wengi bado hawamudu
kulipia.
Amesema hali hiyo imefanya idadi kubwa ya wana TBN kushindwa
kumudu kuendesha mitandao yao kutoka 300+ waliokuwapo kwanza hadi kufikia 100+
tu wanaoweza kulipia na kwa kusuasua.
Ameshauri pia TCRA kuendeleza utamaduni wa kukutana na wadau
wake ikiwamo kwa mafunzo ya kuwaimarisha uwezo wao pamoja na kuangazia athari
za gharama za bando za mtandao na vifaa.
Amesema ikiwa sekta ya blogging ndani ya tasnia ya habari
ikisimamiwa vizuri kwa ushirikiano wa karibu na TCRA ni wazi kwamba Tanzania
itanufaika na maudhui bora na yenye viwango ambayo yatasaidia kulinda maadili
ya jamii yetu.
TBN yenye wanachama 300 waliopo wanaendesha mitandao kwa
kusuasua kutokana na ada na tozo.
Watalaam hao walionesha kushangazwa na kuwapo kwa Chama Cha
Bloggers chenye usajili kamili na wanachama zaidi ya 300, na pia wakaelewa
bloggers ni tofauti na jumuiya zingine za waandishi wa mitandao ambao hawana
blogs.
Wataalamu hao ni pamoja na Prof. Siasa Mzenzi, Dkt. Patrokil
Kanje , Dkt. Said Suluo.
Wengine ni Mjata Daffa , Ally Mshana na Viongozi na wajumbe
wa TBN, wakiongozwa na Katibu Mtendaji Khadija Kalili, Beda Msimbe na Rahel
Pallangyo.


0 Maoni