Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa
amewataka Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji kutekeleza majukumu yao kwa
uzalendo, uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaweza
kupelekea uingiaji wa wahamiaji haramu nchini.
Bashungwa ameeleza hayo jana katika kikao kazi na Maafisa na
Askari wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika wilaya ya Karagwe, Mkoa wa
Kagera.
“Wizara itawasimamia kikamilifu maafisa Uhamiaji katika
kutekeleza majukumu yao. Wale ambao watakosa uzalendo na uadilifu, na kuwa
sehemu ya chanzo cha kuchochea uingiaji wa wahamiaji haramu kwa lengo la
kujipatia fedha au rushwa, tutawachukulia hatua kali za kisheria na za
kiutumishi,” amesema Bashungwa.
Bashungwa amesema Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa Mikoa
ambayo iko mipakani, ambao umekuwa ukikumbwa na changamoto ya baadhi ya wageni
kutoka nchi jirani kuingia kinyume na taratibu kutokana na ukubwa wa mpaka.
Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa viongozi wa vijiji na kata,
kuwa mstari wa mbele kusimamia ili kukomesha suala la uhamiaji haramu bila
kumuonea au kumkomoa mtu kwa kutoa taarifa kwa maafisa wa uhamiaji pale
zinapohitajika.
Amewahimiza wananchi kutoa taarifa pindi watakapoona Askari
wa Idara ya Uhamiaji anafanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili, sheria na
taaluma yake ili kuhakikisha kila mgeni anayeingia nchini anaingia kwa mujibu
wa sheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Julius Laiser ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuviwezesha vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Idara ya Uhamiaji Wilaya ya Karagwe kupewa gari jipya.



0 Maoni