WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasihi viongozi wa dini
nchini waendelee kukemea vikali vitendo vyote ambavyo ni kinyume na maadili ya
dini na utamaduni wa Mtanzania.
"Ninawaomba viongozi wetu wa dini tuendelee kuliweka
suala la kuimarisha malezi na kidhibiti mmomonyoko wa maadili kuwa ajenda ya
kudumu. Lazima tuwe na maadili mema ili Taifa liwe endelevu".
Ametoa rai hiyo leo (Jumapili Machi 9, 2025) alipomwakilisha
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu na
kutawazwa kwa Askofu wa Pili wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kiteto, Askofu
Bethuel Mlula iliyofanyika anisa Kuu la Anglikana la Mtakatifu Mikaeli, Kiteto
Mkoani Manyara.
Aidha, Waziri Mkuu amesema pamoja na masuala ya kiroho
amewaomba viongozi wa dini waendelee kuwahamasisha waumini kuunga mkono ajenda
mbalimbali za kitaifa, ikiwemo ya uhifadhi wa mazingira, kampeni ya nishati
safi na upandaji miti pamoja na kushiriki katika hatua zote za uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Askofu wa
kwanza mstaafu wa Kanisa hilo Askofu Isaiah Chambala kwa kazi kubwa aliyoifanya
katika kipindi cha uongozi wake, pia ametumia fursa hiyo kumhakikishai
ushirikiano wa kutosha kwa mslahi mapana ya Wana-Kiteto na Watanzania kwa
ujumla.
“Nitumie nafasi hii kuwahakikishia viongozi wetu wa dini
kwamba Serikali ipo pamoja nanyi, tutaendelea kuwa na vikao vya pamoja na sisi
tunathamini sana namna ambavyo mmejitoa kuiunga mkono Serikali hii.”
Kwa upande wake, Askofu Mlula ameipongeza Serikali ya Awamu
ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa jitihada kubwa
zinazofanyika ili kuwaletea Watanzania maendeleo katika sekta mbalimbali nchini
ikiwemo afya na elimu.
Aidha, Askofu Mlula ameipongeza Serikali kwa kusimamia amani
umoja na utulivu ambayo iliasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na
Sheikh Abeid Amani Karume. “Amani ni tunu ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia,
tuitumie amani hii kujiletea maendeleo”.
Naye, Askofu wa Tanga na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Mhashamu Maimbo Mndolwa ametoa wito kwa wakazi wa Kiteto kwenda kuhakiki majina yao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki uchaguzi mkuu wa wabunge na madiwani. “Haki ya jina kuwepo kwenye daftari ni yako ila unaweza ipoteza usipoitumia vizuri, tushiriki katika michakato iliyoandliwa na Serikalil.”




0 Maoni