Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imesisitiza jamii kutumia barabara kwa
kuzingatia matumizi sahihi, na kuwataka baadhi ya wananchi kuacha tabia ya kutupa
taka barabarani kwani barabara sio jalala.
Akiongea katika
semina ya Waandishi wa Habari wa Mitandao ya Jamii jana Jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira na Jamii wa TARURA, Mhandisi Heladius Makene, amesema
kumekuwa na matumizi mabaya ya barabara ambayo hayazingatii uzalendo.
“Wananchi hawapaswi
kutupa chupa ama taka za aina yotote barabarani, jambo hilo husababisha
uharibifu wa barabara pale taka zinapoziba kwenye mtaro na kuisababishia hasara
serikali na jamii inayotumia barabara husika,” alisema Mhandisi Makene na
kuongeza,
“Barabara
inapoharibika jamii ya eneo hilo wanakosa mawasiliano, wanashindwa kufikia
huduma za msingi za kijamii kama vile nyumba za ibada, huduma za afya na elimu
pamoja na masoko, pia hata bidhaa bei zake hupanda na kuongeza makali ya maisha.”
Amesema mbali
na utupaji taka pia kumekuwapo na mtindo wa kuvamia njia za watembea kwa miguu
na hata kwenye service road na kutumika kama sehemu za kufanyia biashara jambo ambalo ni kosa na si matumizi sahihi ya
barabara.
“Wafanyabiashara
wanavamia njia za watembea kwa miguu na kufanya biashara na kusababisha kero
kwa watembea kwa miguu…wanasahau kwamba sisi sote ni watembea kwa miguu na kuna
wakati tuhahitaji kutumia njia hizo,” alisema Mhandisi Makene.
Amesema
kwamba, “Kwa mfano Kariakoo wafanyabiashara wamevamia barabara na kusababisha tabu
kwa wanunuzi kuingia na magari yao kwenda kununua bidhaa, jambo hili linaathari
mapato pengine kungekuwa panapitika wanunuzi wangekuja wengi kuliko ilivyo sasa.”
Amesema
kwamba kama hiyo haitoshi kuna watu wanahujumu miundombinu ya barabara kwa
kuiba vyuma vya alama za barabarani, kingo za madaraja, taa na hata wengine
wamefikia hatua ya kuziponda nguzo za mipaka ili watoe nondo wakauze.
Kwa kutambua
tatizo hilo Mhandisi Makene amesema kwamba TARURA kwa kushirikiana na wadau
wengine hivi karibuni wanatarajia kuzindua kampeni kubwa ya kitaifa itakayokuwa
inajulikana kwa jina la “Barabara Sio Jalala”.
Semina hiyo
iliyowahusisha Jumuiya ya Wanahabari Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA),
ilifunguliwa na Meneja wa TARURA Kingamboni Mhandisi Ismail Mafita kwa niaba ya
Mtendaji Mkuu wa TARURA Victor Seff.
0 Maoni