WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi imara ambaye amedhamiria kuwahudumia
Watanzania kwa kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia katika maeneo yao.
Amesema hayo kwa nyakati tofauti wakati alipoweka mawe ya
msingi ya Miradi ya Upanuzi wa Mtandao wa Majisafi ya Ziwa Victoria kutoka Ziba
hadi Nkinga na Makomero hadi Mgongoro, wilayani Igunga mkoani Tabora, Machi 12,
2025.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa Ziba
hadi Nkinga unaogharimu shilingi bilioni 2.49 na kutarajia kuhudumia wananchi
32,979, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kusimamia utoaji
wa huduma za maji safi na salama nchini ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia
wananchi kwa asilimia 100.
“Ndugu zangu wananchi, mradi huu ni matokeo ya utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, kuweni na uhakika kwamba Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan ni kiongozi
anayewajali, anawapenda na anasikiliza changamoto zenu, endeleeni
kutekeleza majukumu yenu ipasavyo kwasababu tunaye kiongozi madhubuti.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania
kulinda mazingira na vyanzo vya maji ili
vitumike ili viweze kutoa huduma endelevu ya maji. “Tunamshukuru Rais Dkt.
Samia kwa kuongeza bajeti ili wizara ya maji imudu kupeleka maji hadi vijijini
lengo ni wananchi wapate maji kwenye maeneo yote.”
“Mkurugenzi hakikisha
unaanza ujenzi wa zahanati katika eneo hili, sio sawa wakazi wa eneo hili
kutembea umbali wa takribani kilomita 20 kufuata huduma.”
Akizungumza wakati akikagua vibanda vya biashara
vilivyojengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Waziri Mkuu amewataka
watendaji wa Halmashauri hiyo kutafuta njia nzuri ambayo itawawezesha
wafanyabiashara kunufaika na uwepo wa vibanda hivyo badala ya kutumia utaratibu
wasasa.
"Ninawapongeza sana kwa uamuzi wa ujenzi wa vibanda hivi, ni jambo kubwa ambalo litawawezesha wafanyabiashara wetu kuwa na maeneo ya uhakika ya ufanyaji wa biashara, lakini angalieni huu mfumo wenu, oneni namna mtakavyoweza kutafuta utaratibu mzuri wa kuwapatia wafanyabiashara.”
0 Maoni