Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) imetembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi iliyojengwa
kwa kutumia teknolojia mbadala jijini Dodoma.
Miradi hiyo ni ujenzi wa barabara Km. 6.95 kwa kutumia teknolojia ya ‘Ecoroads’
iliyopo wilayani Chamwino pamoja na ujenzi wa daraja la mawe la Nghong’ona
lenye urefu wa mita 26.44 na upana wa mita 7 lililopo kata ya Nghong’ona jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi
Mhandisi Florian Kabaka amesema kuwa, lengo la kukagua miradi hiyo ni kuona
utendaji wa teknolojia mbadala ili kuona kama inafaa kutumika katika maeneo
mengine nchini.
“Teknolojia hii ni mpya kwetu hivyo ni muhimu tuangalie na
kukagua mara kwa mara kuona kama zinatufaa ama la, kwa upande wa teknolojia ya
‘Ecoroads’ ndio tumeanza kuitumia na barabara ina miezi 7, kwa mazingira na
udongo wa nchi yetu bado tunahitaji kujifunza zaidi tuone kama inafaa kwetu,” amesema.
Kuhusu ubora wa madaraja ya mawe, Mhandisi Kabaka ameeleza
kuwa yanafanya vizuri na yanatumia gharama ndogo, ukilinganisha na madaraja ya
zege na nondo ambapo na hivyo amewataka TARURA kufanya usimamizi na ufuatiliaji
wa mara kwa mara wa miundombinu hiyo.
Aidha, Mhandisi Kabaka ametoa wito kwa wananchi kuilinda
miundombinu iliyopo kwenye maeneo yao ili iweze kudumu kwa muda mrefu, aidha,
amewataka wananchi watoe taarifa mapema kama kukitokea uharibifu wa miundombinu
katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma, Mhandisi
Edward Lemelo amesema teknolojia ya ‘Ecoroads’ ni kemikali zinazochanganywa
kwenye udongo ili kupunguza gharama katika ujenzi wa barabara ambapo
wanaendelea kufanya ufuatiliaji ili kuona ubora wa teknolojia hiyo kwa lengo la
kutumia katika kazi zao kwa ujumla.
Ameongeza kuwa madaraja ya mawe wameona yanapunguza gharama na mpaka sasa katika mkoa wa Dodoma wamejenga madaraja 9 huku madaraja 8 ujenzi wake ukiwa unaendelea na mpango kwa mwaka ujao wa fedha ni kujenga madaraja makubwa 2 ambapo kwa kipindi kifupi watakuwa wamejenga madaraja 19 ya mawe.
0 Maoni