Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Urusi
katika sekta ya misitu kwa lengo la kuboresha uhifadhi wa rasilimali zake
kupitia teknolojia na mbinu za kisasa.
Hayo yamejiri katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Balozi Pindi Chana (Mb) na
wataalamu wa misitu kutoka Urusi waliotembelea Wizara ya Maliasili na Utalii
jijini Dodoma leo Machi 12,2025 ambapo majadiliano yao yalilenga kuboresha
sekta ya misitu kupitia tafiti na ushirikiano wa kiteknolojia.
Katika kikao hicho, kilichoshirikisha pia maofisa wa taasisi
za sekta ya misitu wakiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Waziri Chana alieleza
kuwa Tanzania ina eneo la misitu lenye takriban hekta milioni 48.1, sawa na
asilimia 55 ya ardhi ya taifa na kwamba misitu hiyo ina mchango mkubwa katika
mazingira, jamii, na uchumi wa nchi.
Hata hivyo, Mhe. Chana alionyesha wasiwasi wake kuhusu
changamoto zinazoikumba misitu nchini, ikiwemo ongezeko la mahitaji ya mazao ya
misitu, upanuzi wa shughuli za kilimo, na ongezeko la makazi ya watu na
kusisitiza kuwa ushirikiano na Urusi utasaidia kukabiliana na changamoto hizo
kwa kutumia teknolojia za kisasa kama uchunguzi wa mbali, mifumo ya taarifa za
kijiografia (GIS), na mbinu bunifu za uhifadhi.
Alifafanua kuwa hatua hiyo ni sehemu ya uhusiano wa muda
mrefu kati ya Tanzania na Urusi, ambao ulianza tangu mwaka 1960 na pia alitaja
mchango wa taasisi za ndani kama Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),
Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), na vyuo maalumu vya mafunzo ya
misitu kama Chuo cha Mafunzo ya Misitu (FTI) na Chuo cha Mafunzo ya Viwanda vya
Misitu (FITI).
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ufundi wa
Misitu cha Jimbo la Saint Petersburg, Profesa Alexander Dobrovolsky, alisema
kuwa Tanzania ina bioanuwai tajiri inayofaa kwa tafiti za ikolojia na mafunzo
ya wanafunzi wa Urusi.
Aliongeza kuwa Urusi itashirikiana na Tanzania kwa kutumia
teknolojia za kisasa kama droni kwa ufuatiliaji wa misitu, kuzuia moto wa
misitu, na kudhibiti wadudu waharibifu. Pia alitangaza kuwa chuo hicho kitatoa
droni, mafunzo, na programu za kusaidia sekta ya misitu ya Tanzania.
Kwa kuhitimisha, Waziri Chana alieleza kuwa ziara hiyo ni hatua muhimu katika juhudi za Tanzania kuboresha uhifadhi wa misitu na kuhakikisha rasilimali hizi zinanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo kwa njia endelevu.
0 Maoni