WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Machi 05, 2025 ameweka jiwe
la msingi la ujenzi wa mradi wa Bwawa la Kidunga litakalokuwa na uwezo wa
kuhifadhi maji lita bilioni 190.
Ujenzi wa Bwawa hilo ambalo hadi kukamilika kwake
litagharimu shilingi bilioni 335.8 ikiwa ni fedha za ndani umefikia asilimia 28
za utekelezaji.
Lengo la mradi huo ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa
maji kwa muda wote katika mto Ruvu na hivyo kufanya uwepo wa maji ya uhakika
kwa jiji la Dar es Salaam, mkoa wa Pwani na Morogoro.
Vilevile, mradi huo unatarajiwa kuwa na mtambo wa uzalishaji
umeme megawati 20, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita
101 kutoka Kidunda hadi Chalinze kwenye gridi ya Taifa pamoja na ujenzi wa
barabara kiwango cha Changarawe yenye urefu wa kilomita 75 kutoka Ngerengere
hadi Kidunda.
Mradi huo utakapokamilika unatarajia Kuboresha huduma ya Majisafi kwa ajili ya matumizi ya Majumbani, Kilimo na Viwanda kwa kuhakikisha upatikanaji wa muda wote katika mto Ruvu kwa kutiririsha wastani wa lita 24,000 kwa sekunde zitakazokidhi mahitaji ya maji hususani kwenye kipindi cha ukame.



0 Maoni