Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Kabange leo 11 Machi, 2025 amefungua rasmi
kikao kazi cha maandalizi ya bajeti ya TAWA kwa Mwaka wa fedha 2025/2026
kilichofanyika katika ukumbi wa Ngorongoro jijini Arusha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Kamishna
Kabange amesema maksio ya bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 yanapaswa
kujielekeza katika vipaumbele vya Mamlaka ambavyo ni pamoja na ulinzi wa
rasilimali za wanyamapori na malikale, utatuzi wa migogoro ya mipaka na
udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu pamoja, kuimarisha utalii na
kuongeza mapato pamoja pamoja na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa
watumishi.
"Katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori nawaelekeza
kuendelea kuimarisha ulinzi wa maeneo yetu ya hifadhi ikiwa ni pamoja na
kuendelea kusimamia kikamilifu masuala ya doria," amesema Kamishna
Kabange.
Kadhalika, Kamishna Kabange amewaelekeza Makamanda wa Kanda
kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza idadi ya watalii pamoja na mapato.
Pamoja na hilo, Makamanda wa Kanda wametakiwa kuhakikisha
watumishi wanazingatia sheria, kanuni zilizopo sambamba na taratibu za kijeshi
ili kudumisha nidhamu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
Pia ameelekeza utunzaji wa vitendea kazi yakiwemo magari ya doria na miundombinu mbalimbali iliyojengwa katika maeneo wanayosimamia.
Na. Joyce Ndunguru - Arusha




0 Maoni