Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa
Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Augustine Vuma amesema kukamilika kwa Jengo la Ofisi
Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA), kutaongeza morali ya watumishi katika utendaji
kazi hivyo kuboresha zaidi huduma zake kwa wananchi.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari, Machi 13, 2025
baada ya Kamati hiyo kuzuru na kujionea Jengo hilo jipya la kisasa lililojengwa
na kampuni ya wakandarasi wazawa ijulikanayo kama Ms. Mohammedi Builders Ltd
kwa gharama ya shilingi za kitanzania bilioni 6.1.
“Ujio wa Mradi huu unaamsha ari ya kufanya kazi kwa
watumishi na ubunifu zaidi, jambo ambalo tunaamini litaongeza tija kwa maana ya
makusanyo ya Wakala, lakini pia miradi itaenda kuwasaidia Watanzania kulindwa
vizuri dhidi ya watu wasio waaminifu ambao huwapunja wananchi kwenye vipimo
mbalimbali,” amesema Mhe. Vuma.
Aidha, Mhe. Vuma ametoa pongezi kwa Serikali chini ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha
upatikanaji wa fedha za ujenzi wa jengo hilo.
Vilevile ametoa pongezi kwa Waziri wa Viwanda na Biashara,
Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Menejimenti yote ya Wizara pamoja na Uongozi wa WMA
kwa usimamizi mzuri uliowezesha kufanikisha ujenzi husika.
Katika hatua nyingine, Mhe. Vuma amempongeza Mkandarasi wa
jengo hilo na kutoa rai kwa Serikali pamoja na wadau wengine kuendelea
kuwaamini wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mbalimbali ili fedha wanazolipwa
ziendelee kubaki nchini na kuchangia katika kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na
Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Samia kuwezesha
ujenzi huo, pia amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutawezesha kutimiza
maono yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Hashil ameiahidi Kamati ya Bunge kutimiza maelekezo
waliyoyatoa, hususan yanayohusu Wizara na WMA kuutumia muda wa mwaka mmoja wa
matazamio ya jengo kwa kuhakikisha dosari ndogo ndogo zitakazojitokeza
zinarekebishwa.
Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari kuhusu
kuanza kutumika kwa jengo, Katibu Mkuu amebainisha kuwa tayari makabidhiano
yalikwishafanyika na kwamba utaratibu wa kuhamisha watumishi umekwishaanza.
Ujenzi wa Jengo hilo ulianza kutekelezwa Julai 2022 ambapo
imeelezwa kuwa kukamilika kwake kutaokoa matumizi ya kiasi kikubwa cha fedha
kilichokuwa kinalipwa kama kodi ya pango kutokana na Wakala kutumia majengo ya
kukodi kwa ajili ya Ofisi yake kuu kwa muda mrefu.
Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo umesimamiwa na Mshauri Elekezi Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).



0 Maoni