Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar na Chama cha waongoza
watalii Zanzibar (ZATO) wafanya ziara maalumu (Fam - Trip) katika Hifadhi ya
urithi wa utamaduni wa dunia Magofu ya Kale Kilwa Kisiwani na Songo Mnara
Mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kupanua wigo wa soko la utalii
katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara
Kwa lengo la kukuza vivutio vya kihistoria na asili ili kuvutia watalii
wengi zaidi.
Ziara hiyo iliyofanyika jana Februari 6, iliratibiwa na
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania - TAWA inalenga kuimarisha
ushirikiano kati ya Zanzibar na maeneo mengine ya bara yaliyo chini ya
usimamizi wa TAWA na kuwawezesha wadau hao kuona vivutio vya utalii na fursa za
uwekezaji pamoja na kujadili masuala ya
kukuza na kutangaza utalii wa kimataifa.
Majadiliano na wadau hao wa Sekta ya utalii yaliwahusisha
wawakilishi kutoka TAWA ambayo iliwakilishwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi
Kitengo cha Biashara Hamza Hassan,
Mohammed Walid Fikirin kutoka Kamisheni ya utalii Zanzibar na Thabit Abdulrazak
Abdulrahman wa ZATO.
Aidha, majadiliano hayo yalijikita katika kusuka mikakati ya
kutangaza vivutio vya Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia Magofu ya Kilwa
Kisiwani na Songo Mnara, Pori la Akiba Pande na Hifadhi ya Magofu ya Kale
Kunduchi pamoja na Pori la Akiba Wami-Mbiki Kwa lengo la kuvutia watalii kutoka
pembe zote za dunia.
Hii ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA kuunganisha Zanzibar na vivutio vya utalii vilivyopo mikoa ya Tanzania Bara ikiwa ni hatua muhimu katika kutangaza utalii wa kiutamaduni, kihistoria na wa asili huku zikiweka misingi ya kukuza uchumi wa Taifa Kwa njia endelevu.
Na. Beatus Maganja - Kilwa




0 Maoni