Wathaminishaji madini watakiwa kuwa waadilifu na kuepuka makosa

 

Wathaminishaji wa madini wametakiwa kuwa waadilifu na kutumia taaluma yao vizuri ili kuepuka makosa madogo madogo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa Tume ya Madini, Nsajigwa Kabigi wakati akifungua kikao cha wathaminishaji wa madini kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini,  Mhandisi Ramadhani Lwamo kinachoendelea jijini Dodoma.

Amesema kazi ya uthaminishaji madini inahitaji umakini mkubwa kwa mthaminishaji kutambua vizuri aina ya madini na kutoa thamani halisi.

"Sasa ikitokea kwa bahati mbaya  ukatoa thamani kiasi fulani baadaye ikaenda kuthaminishwa sehemu nyingine na kuonekana ni tofauti inaharibu  sifa yako na uadilifu wako unakuwa na maswali,  hivyo tujitahidi  kutumia taaluma zetu vizuri ili hata ikitokea iwe ni makosa ya kibinadamu na sio uzembe," amesema Kabigi.

Katika hatua nyingine, Kabigi amewataka wathaminishaji madini kujiendeleza kimasomo ikiwa ni pamoja na kutafuta taarifa mbalimbali zinazotokana na kazi zao ndani na nje ya nchi pamoja na kushirikishana uzoefu.

"Ni wajibu wetu sisi kama mwajiri kuwaendeleza nyie ili kuendana na teknolojia mpya na mabadiliko mbalimbali ambayo yamekuwepo," amesema Bw. Kabigi.

Awali akizungumza Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya madini CPA. Venance Kasiki amesema lengo la kikao hicho ni kujengeana uwezo na kukumbushana majukumu kwa wathaminishaji madini ili kuendana na teknolojia inavyokuwa.




Chapisha Maoni

0 Maoni