Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika
mkoani Tanga na Pwani kwa siku saba kuanzia tarehe 13 hadi 19 Februari, 2025
ambapo wapiga kura wapya 431,016 wanatarajiwa kuandikishwa na zoezi hilo
litakapokamilika mikoa hiyo itakuwa na wapiga kura 2,727,318.
Akifungua mkutano wa wadau mkoani Tanga, Mwenyekiti wa Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa, Jacobs Mwambegele leo Januari 02,
2025 amesema mkoani Pwani zoezi hilo litafanyika kwa mkoa mzima na mkoani Tanga
litajumuisha Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri za Miji ya
Handeni na Korogwe na Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Lushoto na Muheza.
“Leo tupo hapa Tanga na wenzetu wapo mkoa wa Pwani ikiwa ni
maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hii, ambapo zoezi litafanyika
kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 13 Februari, 2025 na kukamilika tarehe 19
Februari, 2025 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na
kufungwa saa 12:00 jioni,” amesema Jaji Mwambegele.
Akifungua mkutano kama huo mkoani Pwani, Makamu Mwanyekiti
wa Tume, Mhe. Jaji Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk amesema tayari Tume
imeshakamilisha zoezi hilo kwenye mikoa 25 na kwamba mikoa ya Lindi, Mtwara na
sehemu ya Mkoa wa Ruvuma inakamilisha zoezi hilo Februari 03, 2025.
Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Kigoma, Tabora, Katavi, Geita,
Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma, Singida, Mjini
Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba,
Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe na Ruvuma.
“mikoa miwili ya Mtwara na Lindi na sehemu ya mkoa wa Ruvuma
kwenye halmashauri za Madaba, Namtumbo na Tunduru inatarajia kukamilisha zoezi
hilo tarehe 03 Februari, 2025,” amesema.
Mada ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ndugu. Kailima
Ramadhani ambayo ameiwasilisha mkoani Tanga na ambayo imewasilishwa kwa niaba
yake Mkoani Pwani na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria, Ndugu. Selemani Mtibora
imeeleza kuwa wapiga kura wapya 431,016 wanatarajiwa kuandikishwa na zoezi hilo
litakapokamilika mikoa hiyo itakuwa na wapiga kura 2,727,318 sawa na ongezeko
la asilimia 18.7 ya wapiga kura 2,296,302 waliopo kwenye daftari katika mikoa
hiyo.
“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo
watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa
uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine
hawakuweza kujiandikisha,” imesema sehemu ya nada hiyo.
0 Maoni