UZALISHAJI wa madini
ya makaa ya mawe katika kijiji cha Ntunduwaro kata ya Ruanda wilayani
Mbinga ni chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali na maendeleo
ya wananchi wa kata hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Meneja wa Mgodi wa
Market Insight Limited (MILCOAL), Atit
Mehta amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 mgodi huo umeweza kuilipa serikali Shilingi Bilioni 5.2 kutokana na mrabaha, tozo na ada
mbalimbali.
Kuhusu Kampuni hiyo kuwajibika kwa jamii inayozunguka mradi
kwa maana ya CSR, Mehta amesema wamekuwa wakitekeleza kwa uaminifu Sera ya Madini inayotambua uwajibikaji wa
Kampuni kwa jamii zinazozunguka miradi
na mgodi wao wameweza kujenga barabara ya kutoka Ntunduwaro mpaka Liyumbi yenye
urefu wa Kilomita 23.
“Kwa sasa tunamalizia mchakato wa mwisho na viongozi wa
Serikali akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) tuweze kujenga Zahanati Ntunduwaro
ili kuleta unafuu wa matibabu kwa wananchi wa
kijiji hiki,”amesema.
Aidha, amesema kampuni hiyo ya MILCOAL imetoa ajira kwa watu
200 kati yao tisa ni wenye asili ya Kihindi na waliosalia ni wazawa.
Naye, Mjiolojia Abraham Nkya akizungumza kwa niaba ya Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, amesema mgodi huo wa MILCOAL ambao upo mkoani
Njombe ukiwa unapakana na wilaya ya Mbinga ndio unaochangia kiasi kikubwa cha
mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini kwenye mkoa huo.
“Madini ya Makaa ya Mawe ndio yanayoongoza kwa kutupa mapato makubwa, mwaka wa fedha uliopita wa
2023/2024 madini ya makaa ya mawe pekee
yaliingiza kiasi cha shilingi
bilioni 4.155 na kuufanya Mkoa wa Njombe kuchangia vizuri
mapato ya Serikali,”amesema.
Kwa upande wake Mjiolojia kutoka MILCOAL, Cyprian Ndaza ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wawekezaji ili ajira zaidi ziweze kutolewa kwa wazawa.


0 Maoni